Translations Suras
KISWAHILI

83 - AL - MUT'AFFIFIIN

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

 
1Ole wao hao wapunjao!
 
2Ambao wanapo jipimia kwa watu hudai watimiziwe.
 
3Na wao wanapo wapimia watu kwa kipimo au mizani hupunguza.
 
4Kwani hawadhani hao kwamba watafufuliwa
 
5Katika Siku iliyo kuu,
 
6Siku watapo msimamia watu Mola Mlezi wa walimwengu wote?
 
7Hasha! Hakika maandiko ya wakosefu bila ya shaka yamo katika Sijjin.
 
8Unajua nini Sijjin?
 
9Kitabu kilicho andikwa.
 
10Ole wao siku hiyo kwa wanao kadhibisha!
 
11Ambao wanaikadhibisha Siku ya Malipo.
 
12Wala haikadhibishi ila kila mwenye kuruka mipaka, mwenye dhambi.
 
13Anapo somewa Aya zetu husema: Ni visa vya watu wa kale!
 
14Hasha! Bali yametia kutu juu ya nyoyo zao hao walio kuwa wakiyachuma.
 
15Hasha! Hakika hao siku hiyo bila ya shaka watazuiliwa na neema za Mola wao Mlezi.
 
16Kisha wataingia Motoni!
 
17Kisha waambiwe: Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyakadhabisha.
 
18Hasha! Hakika maandiko ya watu wema bila ya shaka yamo katika I'liyyin.
 
19Na nini kitakacho kujuvya nini I'liyyin?
 
20Kitabu kilicho andikwa.
 
21Wanakishuhudia walio karibishwa.
 
22Hakika watu wema bila ya shaka watakuwa katika neema.
 
23Wakae juu ya viti vya enzi wakiangalia.
 
24Utatambua katika nyuso zao mng'aro wa neema,
 
25Watanyweshwa kinywaji safi kiliyo tiwa muhuri,
 
26Muhuri wake ni miski. Na katika hayo washindanie wenye kushindana.
 
27Na mchanganyiko wake ni Tasniim,
 
28Chemchem watakayo inywa walio kurubishwa.
 
29Kwa hakika wale walio kuwa wakosefu walikuwa wakiwacheka walio amini.
 
30Na wanapo pita karibu yao wakikonyezana.
 
31Na wanapo rudi kwa watu wao hurudi nao wamefurahi.
 
32Na wanapo waona husema: Hakika hawa ndio khasa walio potea.
 
33Na wao hawakutumwa wawe walinzi juu yao.
 
34Basi leo walio amini ndio watawacheka makafiri,
 
35Nao wako juu ya viti vya enzi wakiangalia.
 
36Je! makafiri wamelipwa malipo ya yale waliyo kuwa wakiyatenda?
 
 
ReadTheQuran.org