Translations Suras
KISWAHILI

80 - A'BASA

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

 
1Alikunja kipaji na akageuka,
 
2Kwa sababu alimjia kipofu!
 
3Na nini kitakujuulisha pengine yeye atatakasika?
 
4Au atawaidhika, na mawaidha yamfae?
 
5Ama ajionaye hana haja,
 
6Wewe ndio unamshughulikia?
 
7Na si juu yako kama hakutakasika.
 
8Ama anaye kujia kwa juhudi,
 
9Naye anaogopa,
 
10Ndio wewe unampuuza?
 
11Sivyo hivyo! Huku ni kukumbushana.
 
12Basi anaye penda akumbuke.
 
13Yamo katika kurasa zilizo hishimiwa,
 
14Zilizo inuliwa, zilizo takaswa.
 
15Zimo mikononi mwa Malaika waandishi,
 
16Watukufu, wema.
 
17Ameangamia mwanaadamu! Nini kinacho mkufurisha?
 
18Kwa kitu gani amemuumba?
 
19Kwa tone la manii, akamuumba na akamkadiria.
 
20Kisha akamsahilishia njia.
 
21Kisha akamfisha, akamtia kaburini.
 
22Kisha apendapo atamfufua.
 
23La! Hajamaliza aliyo muamuru.
 
24Hebu mtu na atazame chakula chake.
 
25Hakika Sisi tumemimina maji kwa nguvu,
 
26Tena tukaipasua pasua ardhi kwa nguvu,
 
27Kisha tukaotesha humo nafaka,
 
28Na zabibu, na mimea ya majani,
 
29Na mizaituni, na mitende,
 
30Na bustani zenye miti iliyo songana baraabara,
 
31Na matunda, na malisho ya wanyama;
 
32Kwa manufaa yenu na mifugo yenu.
 
33Basi utakapo kuja ukelele,
 
34Siku ambayo mtu atamkimbia nduguye,
 
35Na mamaye na babaye,
 
36Na mkewe na wanawe -
 
37Kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na lake la kumtosha.
 
38Siku hiyo ziko nyuso zitazo nawiri,
 
39Zitacheka, zitachangamka;
 
40Na nyuso siku hiyo zitakuwa na mavumbi,
 
41Giza totoro litazifunika,
 
42Hao ndio makafiri watenda maovu.
 
 
ReadTheQuran.org