Translations Suras
KISWAHILI

79 - ANNAZIA'AT

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

 
1Naapa kwa wanao komoa kwa nguvu,
 
2Na kwa wanao toa kwa upole,
 
3Na wanao ogelea,
 
4Wakishindana mbio,
 
5Wakidabiri mambo.
 
6Siku kitapo tetemeka cha kutetemeka,
 
7Kifuate cha kufuatia.
 
8Siku hiyo nyoyo zitapiga piga,
 
9Macho yatainama chini.
 
10Sasa wanasema: Ati kweli tutarudishwa kwenye hali ya kwanza?
 
11Hata tukiwa mifupa iliyo bunguliwa?
 
12Wanasema: Basi marejeo hayo ni yenye khasara!
 
13Kwa hakika hayo ni ukelele mmoja tu,
 
14Mara watakuwa kwenye uwanda wa mkutano!
 
15Je! Imekufikia hadithi ya Musa?
 
16Mola wake Mlezi alipo mwita katika bonde takatifu la T'uwaa, akamwambia:
 
17Nenda kwa Firauni. Hakika yeye amezidi jeuri.
 
18Umwambie: Je! Unapenda kujitakasa?
 
19Nami nitakuongoa ufike kwa Mola wako Mlezi, upate kumcha.
 
20Basi alimwonyesha Ishara kubwa.
 
21Lakini aliikadhibisha na akaasi.
 
22Kisha alirudi nyuma, akaingia kufanya juhudi.
 
23Akakusanya watu akanadi.
 
24Akasema: Mimi ndiye Mola wenu Mlezi mkuu kabisa.
 
25Basi hapo Mwenyezi Mungu akamshika kumuadhibu kwa la mwisho na la mwanzo.
 
26Kwa hakika katika haya yapo mazingatio kwa wanao ogopa.
 
27Je! Ni vigumu zaidi kukuumbeni nyinyi au mbingu? Yeye ndiye aliye ijenga!
 
28Akainua kimo chake, na akaitengeneza vizuri.
 
29Na akautia giza usiku wake, na akautokeza mchana wake.
 
30Na juu ya hivyo ameitandaza ardhi.
 
31Akatoa ndani yake maji yake na malisho yake,
 
32Na milima akaisimamisha,
 
33Kwa nafuu yenu na mifugo yenu.
 
34Basi itakapo fika hiyo balaa kubwa,
 
35Siku ambayo mtu atakumbuka aliyo yafanya,
 
36Na Jahannamu itadhihirishwa kwa mwenye kuona,
 
37Basi ama yule aliye zidi ujeuri,
 
38Na akakhiari maisha ya dunia,
 
39Kwa hakika Jahannamu ndiyo makaazi yake!
 
40Na ama yule anaye ogopa kusimamishwa mbele ya Mola wake Mlezi, na akajizuilia nafsi yake na matamanio,
 
41Basi huyo, Pepo itakuwa ndiyo makaazi yake!
 
42Wanakuuliza Saa (ya Kiyama) itakuwa lini?
 
43Una nini wewe hata uitaje?
 
44Kwa Mola wako Mlezi ndio mwisho wake.
 
45Kwa hakika wewe ni mwonyaji tu kwa mwenye kuikhofu.
 
46Ni kama kwamba wao siku watapo iona (hiyo Saa) hawakukaa ila jioni moja tu, au mchana wake.
 
 
ReadTheQuran.org