Translations Suras
KISWAHILI

74 - AL - MUDDATHTHIR

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

 
1Ewe uliye jigubika!
 
2Simama uonye!
 
3Na Mola wako Mlezi mtukuze!
 
4Na nguo zako, zisafishe.
 
5Na yaliyo machafu yahame!
 
6Wala usitoe kwa kutaraji kuzidishiwa.
 
7Na kwa ajili ya Mola wako Mlezi, subiri!
 
8Basi litapo pulizwa barugumu,
 
9Siku hiyo, basi, itakuwa siku ngumu.
 
10Kwa makafiri haitakuwa nyepesi.
 
11Niache peke yangu na niliye muumba;
 
12Na nikamjaalia awe na mali mengi,
 
13Na wana wanao onekana,
 
14Na nikamtgenezea mambo vizuri kabisa.
 
15Kisha anatumai nimzidishie!
 
16Hasha! Kwani hakika yeye alikuwa akizifanyia inadi Aya zetu!
 
17Nitamtesa kwa mateso yasio wezekana.
 
18Kwani hakika yeye alifikiri na akapima.
 
19Basi ameangamia! Vipi alivyo pima!
 
20Tena ameangamia! Vipi alivyo pima!
 
21Kisha akatazama,
 
22Kisha akakunja kipaji, na akanuna.
 
23Kisha akaipa kisogo haki, na akatakabari.
 
24Na akasema: Haya si chochote ila ni uchawi ulio nukuliwa.
 
25Haya si chochote ila kauli ya binaadamu.
 
26Nitakuja mtia kwenye Moto wa Saqar.
 
27Na nini kitakujuulisha ni nini huo Moto wa Saqar?
 
28Haubakishi wala hausazi.
 
29Unababua ngozi iwe nyeusi.
 
30Juu yake wapo kumi na tisa.
 
31Na hatukuwafanya walinzi wa Motoni ila ni Malaika, wala hatukuifanya idadi yao hiyo ila kuwatatanisha walio kufuru, wapate kuwa na yakini walio pewa Kitabu, na wazidi Imani wale walio amini, wala wasiwe na shaka walio pewa Kitabu na Waumini, na wapate kusema wenye maradhi katika nyoyo zao na makafiri: Mwenyezi Mungu amekusudia nini kwa mfano huu? Ndio kama hivyo Mwenyezi Mungu humwacha apotee amtakaye, na humwongoa amtakaye. Na hapana yeyote anaye jua majeshi ya Mola wako Mlezi ila Yeye tu. Na haya si chochote ila ni ukumbusho kwa binaadamu.
 
32Hasha! Naapa kwa mwezi!
 
33Na kwa usiku unapo kucha!
 
34Na kwa asubuhi inapo pambazuka!
 
35Hakika huo Moto ni katika mambo yaliyo makubwa kabisa!
 
36Ni onyo kwa binaadamu,
 
37Kwa anaye taka miongoni mwenu kutangulia au kuchelewa.
 
38Kila nafsi imo rahanini kwa mabaya iliyo yachuma.
 
39Isipo kuwa watu wa kuliani.
 
40Hao watakuwa katika Mabustani, wawe wanaulizana
 
41Khabari za wakosefu:
 
42Ni nini kilicho kupelekeni Motoni?
 
43Waseme: Hatukuwa miongoni walio kuwa wakisali.
 
44Wala hatukuwa tukiwalisha masikini.
 
45Na tulikuwa tukizama pamoja na walio zama katika maovu.
 
46Na tulikuwa tukiikanusha siku ya malipo.
 
47Mpaka yakini ilipo tufikia.
 
48Basi hautawafaa kitu uombezi wa waombezi.
 
49Basi wana nini hata wanapuuza onyo hili?
 
50Kama kwamba wao ni mapunda walio timuliwa,
 
51Wanao mkimbia simba!
 
52Ati kila mmoja katika wao anataka apewe nyaraka zilizo funuliwa.
 
53Hasha! Kwani wao hawaiogopi Akhera?
 
54Hasha! Kwa hakika huu ni ukumbusho!
 
55Basi anaye taka atakumbuka.
 
56Na hawatakumbuka isipo kuwa Mwenyezi Mungu atake. Uchamngu ni kwake Yeye, na msamaha ni wake Yeye.
 
 
ReadTheQuran.org