Translations Suras
KISWAHILI

70 - AL - MAA'RIJ

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

 
1Muulizaji aliuliza juu ya adhabu itakayo tokea,
 
2Kwa makafiri - ambayo hapana awezaye kuizuia -
 
3Kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye mbingu za daraja.
 
4Malaika na Roho hupanda kwendea kwake katika siku ambayo kadiri yake ni miaka khamsini elfu!
 
5Basi subiri kwa subira njema.
 
6Hakika wao wanaiona iko mbali,
 
7Na Sisi tunaiona iko karibu.
 
8Siku ambayo mbingu zitakapo kuwa kama maadeni iliyo yayushwa.
 
9Na milima itakuwa kama sufi.
 
10Wala jamaa hatamuuliza jamaa yake.
 
11Ijapo kuwa wataonyeshwa waonane. Atatamani mkosefu lau ajikomboe na adhabu ya siku hiyo kwa kuwatoa fidia wanawe,
 
12Na mkewe, na nduguye,
 
13Na jamaa zake walio kuwa wakimkimu,
 
14Na wote waliomo duniani, kisha aokoke yeye.
 
15La, hasha! Kwa hakika huo ni Moto mkali kabisa,
 
16Unao babua ngozi ya kichwa!
 
17Utamwita kila aliye geuza mgongo na akageuka.
 
18Na akakusanya mali, kisha akayahifadhi.
 
19Hakika mtu ameumbwa na papara.
 
20Inapo mgusa shari hupapatika.
 
21Na inapo mgusa kheri huizuilia.
 
22Isipo kuwa wanao sali,
 
23Ambao wanadumisha Sala zao,
 
24Na ambao katika mali yao iko haki maalumu
 
25Kwa mwenye kuomba na anaye jizuilia kuomba;
 
26Na ambao wanaisadiki Siku ya Malipo,
 
27Na ambao wanaiogopa adhabu itokayo kwa Mola wao Mlezi.
 
28Hakika adhabu ya Mola wao Mlezi si ya kuaminika nayo.
 
29Na ambao wanahifadhi tupu zao.
 
30Isipo kuwa kwa wake zao, au iliyo wamiliki mikono yao ya kuume, basi hao hawalaumiwi -
 
31Lakini wanao taka kinyume ya haya, basi hao ndio wanao ruka mipaka.
 
32Na ambao wanazichunga amana zao na ahadi zao,
 
33Na ambao wanasimama imara katika ushahidi wao,
 
34Na ambao wanazihifadhi Sala zao.
 
35Hao ndio watakao hishimiwa Peponi.
 
36Wana nini wale walio kufuru wanakutumbulia macho tu?
 
37Makundi kwa makundi upande wa kulia na upande wa kushoto!
 
38Kwani kila mmoja wao anatumai kuingizwa katika Pepo ya neema?
 
39La, hasha! Hakika Sisi tumewaumba kutokana na wanacho kijua.
 
40Basi naapa kwa Mola Mlezi wa mashariki zote na magharibi zote kwamba Sisi tunaweza
 
41Kuwabadili kwa walio bora kuliko wao; na Sisi hatushindwi.
 
42Basi waache wapige porojo na wacheze, mpaka wakutane na siku yao wanayo ahidiwa,
 
43Siku watakapotoka makaburini kwa upesi kama kwamba wanakimbilia mfundo,
 
44Macho yao yatainama, fedheha itawafunika. Hiyo ndiyo Siku waliyo kuwa wakiahidiwa.
 
 
ReadTheQuran.org