Translations Suras
KISWAHILI

69 - AL - H'AAQQAH

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

 
1Tukio la haki.
 
2Nini hilo Tukio la haki?
 
3Na nini kitakujuulisha nini hilo Tukio la haki?
 
4Thamudi na A'di waliukadhibisha Msiba unao situsha.
 
5Basi Thamudi waliangamizwa kwa balaa kubwa mno.
 
6Na ama A'di waliangamizwa kwa upepo mkali usio zuilika.
 
7Alio wapelekea masiku saba, na siku nane, mfululizo bila ya kusita. Utaona watu wamepinduka kama kwamba ni magongo ya mitende yalio wazi ndani.
 
8Basi je! Unamwona mmoja wao aliye baki?
 
9Na Firauni na walio mtangulia, na miji iliyo pinduliwa chini juu, walileta khatia.
 
10Wakamuasi Mtume wa Mola wao Mlezi, ndipo Yeye Mola akawakamata kwa mkamato ulio zidi nguvu.
 
11Maji yalipo furika Sisi tulikupandisheni katika safina,
 
12Ili tuyafanye hayo kuwa ni waadhi kwenu na kila sikio linalo sikia liyahifadhi.
 
13Na litapo pulizwa barugumu mpulizo mmoja tu,
 
14Na ardhi na milima ikaondolewa, na ikavunjwa kwa mvunjo mmoja,
 
15Siku hiyo ndio Tukio litatukia.
 
16Na mbingu zitapasuka, kwani siku hiyo zitakuwa dhaifu kabisa.
 
17Na Malaika watakuwa pembezoni mwa mbingu; na wanane juu ya hawa watakuwa wamebeba Kiti cha Enzi cha Mola wako Mlezi.
 
18Siku hiyo mtahudhurishwa - haitafichika siri yoyote yenu.
 
19Basi ama atakaye pewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, atasema: Haya someni kitabu changu!
 
20Hakika nalijua ya kuwa nitapokea hisabu yangu.
 
21Basi yeye atakuwa katika maisha ya kupendeza,
 
22Katika Bustani ya juu,
 
23Matunda yake yakaribu.
 
24Waambiwe: Kuleni na mnywe kwa furaha kwa sababu ya mlivyo tanguliza katika siku zilizo pita.
 
25Na ama atakaye pewa kitabu chake katika mkono wake wa kushoto, basi yeye atasema: Laiti nisingeli pewa kitabu changu!
 
26Wala nisingeli jua nini hisabu yangu.
 
27Laiti mauti ndiyo yangeli kuwa ya kunimaliza kabisa.
 
28Mali yangu hayakunifaa kitu.
 
29Madaraka yangu yamenipotea.
 
30(Pasemwe): Mshikeni! Mtieni pingu!
 
31Kisha mtupeni Motoni!
 
32Tena mtatizeni katika mnyororo wenye urefu wa dhiraa sabiini!
 
33Kwani huyo hakika alikuwa hamuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu,
 
34Wala hahimizi kulisha masikini.
 
35Basi leo hapa hana jamaa wa kumwonea uchungu,
 
36Wala hana chakula ila usaha wa watu wa Motoni.
 
37Chakula hicho hawakili ila wakosefu.
 
38Basi naapa kwa mnavyo viona,
 
39Na msivyo viona,
 
40Kwa hakika hii ni kauli iliyo letwa na Mjumbe mwenye hishima.
 
41Wala si kauli ya mtunga mashairi. Ni machache sana mnayo yaamini.
 
42Wala si kauli ya kuhani. Ni machache mnayo yakumbuka.
 
43Ni uteremsho utokao kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
 
44Na lau kama angeli tuzulia baadhi ya maneno tu,
 
45Bila ya shaka tungeli mshika kwa mkono wa kulia,
 
46Kisha kwa hakika tungeli mkata mshipa mkubwa wa moyo!
 
47Na hapana yeyote katika nyinyi ambaye angeli weza kutuzuia.
 
48Kwa hakika hii ni mawaidha kwa wachamngu.
 
49Na hakika Sisi bila ya shaka tunajua kwamba miongoni mwenu wapo wanao kadhibisha.
 
50Na hakika bila ya shaka itakuwa ni majuto kwa wanao kataa.
 
51Na hakika hii bila ya shaka ni haki ya yakini.
 
52Basi litakase jina la Mola wako Mlezi Mtukufu.
 
 
ReadTheQuran.org