Translations Suras
KISWAHILI

52 - ATT'UR

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

 
1Naapa kwa mlima wa T'ur,
 
2Na Kitabu kilicho andikwa
 
3Katika ngozi iliyo kunjuliwa,
 
4Na kwa Nyumba iliyo jengwa,
 
5Na kwa dari iliyo nyanyuliwa,
 
6Na kwa bahari iliyo jazwa,
 
7Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi hapana shaka itatokea.
 
8Hapana wa kuizuia.
 
9Siku zitakapo tikisika mbingu kwa mtikiso,
 
10Na milima iwe inakwenda kwa mwendo mkubwa.
 
11Basi ole wao siku hiyo hao wanao kadhibisha,
 
12Ambao wanacheza katika mambo ya upuuzi.
 
13Siku watapo sukumwa kwenye Moto kwa msukumo wa nguvu,
 
14(Waambiwe): Huu ndio ule Moto mlio kuwa mkiukanusha!
 
15Je! Huu ni uchawi, au hamwoni tu?
 
16Uingieni, mkistahamili au msistahamili - ni mamoja kwenu. Hakika mnalipwa kwa mliyo kuwa mkiyatenda.
 
17Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na neema,
 
18Wakifurahi kwa yale aliyo wapa Mola wao Mlezi. Na Mola wao Mlezi atawalinda na adhabu ya Motoni.
 
19Kuleni na kunyweni kwa raha kabisa kwa sababu ya mliyo kuwa mkiyatenda.
 
20Watakuwa wameegemea juu ya viti vya enzi vilivyo pangwa kwa safu. Na tutawaoza mahuru-l-aini.
 
21Na walio amini na dhuriya zao wakawafuata kwa Imani tutawakutanisha nao dhuriya zao, na wala hatutawapunja hata kidogo katika vitendo vyao. Kila mtu lazima atapata alicho kichuma.
 
22Na tutawapa matunda, na nyama kama watavyo penda.
 
23Watapeana humo bilauri zisio na vinywaji vya kuleta maneno ya upuuzi wala dhambi.
 
24Iwe wanawapitia watumishi wao kama kwamba ni lulu zilizomo katika chaza.
 
25Wataelekeana wakiulizana.
 
26Waseme: Tulikuwa zamani pamoja na ahali zetu tukiogopa;
 
27Basi Mwenyezi Mungu akatufanyia hisani na akatulinda na adhabu ya upepo wa Moto.
 
28Hakika sisi zamani tulikuwa tukimwomba Yeye tu. Hakika Yeye ndiye Mwema Mwenye kurehemu.
 
29Basi kumbusha! Kwani wewe, kwa neema ya Mola wako Mlezi, si kuhani wala mwendawazimu.
 
30Au wanasema: Huyu ni mtunga mashairi, tunamtarajia kupatilizwa na dahari.
 
31Sema: Tarajieni, na mimi pia ni pamoja nanyi katika kutarajia.
 
32Au hizo akili zao ndio zinawaamrisha haya, au wao basi ni watu majeuri tu?
 
33Au ndio wanasema: Ameitunga hii! Bali basi tu hawaamini!
 
34Basi nawalete masimulizi kama haya ikiwa wao wanasema kweli.
 
35Au wao wameumbwa pasipo kutokana na kitu chochote, au ni wao ndio waumbaji?
 
36Au wao wameziumba mbingu na ardhi? Bali hawana na yakini.
 
37Au wanazo khazina za Mola wako Mlezi au wao ndio wenye madaraka?
 
38Au wanazo ngazi za kusikilizia? Basi huyo msikilizaji wao na alete hoja ilio wazi!
 
39Au Yeye Mwenyezi Mungu ana wasichana, na nyinyi ndio mna wavulana?
 
40Au wewe unawaomba ujira, na kwa hivyo ndio wanaelemewa na uzito wa gharama?
 
41Au wanayo ilimu ya ghaibu, nao wameandika?
 
42Au wanataka kufanya vitimbi tu? Lakini hao walio kufuru ndio watakao tegeka.
 
43Au wanae mungu asiye kuwa Mwenyezi Mungu? Subhanallah! Ametaksika Mwenyezi Mungu na hao wanao washirikisha naye.
 
44Na hata wange ona pande linatoka mbinguni linaanguka wange sema: Ni mawingu yaliyo bebana.
 
45Basi waache mpaka wakutane na siku yao watakapo hilikishwa.
 
46Siku ambayo hila zao hazitawafaa hata kidogo, wala wao hawatanusuriwa.
 
47Na hakika walio dhulumu watapata adhabu nyengine isiyo kuwa hii, lakini wengi wao hawajui.
 
48Na ingojee hukumu ya Mola wako Mlezi. Kwani wewe hakika uko mbele ya macho yetu, na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi unapo simama,
 
49Na usiku pia mtakase, na zinapo kuchwa nyota.
 
 
ReadTheQuran.org