Translations Suras
KISWAHILI

50 - QAAF

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

 
1Qaaf. Naapa kwa Qur'ani tukufu!
 
2Bali wanastaajabu kwamba amewafikia mwonyaji kutoka miongoni mwao, na wakasema makafiri: Hili ni jambo la ajabu!
 
3Ati tukifa na tukawa udongo...? Kurejea huko kuko mbali!
 
4Hakika Sisi tunajua kiasi cha kila kinacho punguzwa na ardhi kutokana nao. Na kwetu kipo Kitabu kinacho hifadhi yote.
 
5Lakini waliikanusha Haki ilipo wajia; kwa hivyo wamo katika mambo ya mkorogo.
 
6Je! Hawaangalii mbingu zilizo juu yao! Vipi tulivyo zijenga, na tukazipamba. Wala hazina nyufa.
 
7Na ardhi tumeitandaza na tukaiwekea milima, na tukaiotesha mimea mizuri ya kila namna.
 
8Yawe haya ni kifumbua macho na ukumbusho kwa kila mja mwenye kuelekea.
 
9Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji yaliyo barikiwa, na kwa hayo tukaotesha mabustani na nafaka za kuvunwa.
 
10Na mitende mirefu yenye makole yaliyo zaa kwa wingi,
 
11Ili iwe ni riziki kwa waja wangu. Na tukaifufua kwa maji nchi iliyo kuwa imekufa. Kama hivyo ndivyo utakavyo kuwa ufufuaji.
 
12Kabla yao walikadhibisha kaumu ya Nuhu na wakaazi wa Rassi na Thamudi.
 
13Na A'di na Firauni na kaumu ya Lut'i.
 
14Na wakaazi wa Machakani, na watu wa Tubbaa'. Wote hao waliwakanusha Mitume, kwa hivyo onyo likathibitika juu yao.
 
15Kwani tulichoka kwa kuumba mara ya kwanza. Bali wao wamo katika shaka tu juu ya umbo jipya.
 
16Na hakika tumemuumba mtu, nasi tunayajua yanayo mpitikia katika nafsi yake. Na Sisi tuko karibu naye kuliko mshipa wa shingoni mwake.
 
17Wanapo pokea wapokeaji wawili, wanao kaa kuliani na kushotoni.
 
18Hatamki neno ila karibu yake yupo mwangalizi tayari.
 
19Na uchungu wa kutoka roho utamjia kwa haki. Hayo ndiyo uliyo kuwa ukiyakimbia.
 
20Na litapulizwa baragumu. Hiyo ndiyo Siku ya Miadi.
 
21Na kila nafsi itakuja na pamoja nayo mchungaji na shahidi.
 
22(Aambiwe): Kwa hakika ulikuwa umeghafilika na haya; basi leo tumekuondolea pazia lako, na kwa hivyo kuona kwako leo ni kukali.
 
23Na mwenzake atasema: Huyu niliye naye mimi kesha tayarishwa.
 
24Mtupeni katika Jahannamu kila kafiri mwenye inda,
 
25Akatazaye kheri, arukaye mipaka, mwenye kutia shaka,
 
26Aliye weka mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu. Basi mtupeni katika adhabu kali.
 
27Mwenzake aseme: Ee Mola wetu Mlezi! Sikumpoteza mimi, bali yeye mwenyewe alikuwa katika upotovu wa mbali.
 
28(Mwenyezi Mungu) aseme: Msigombane mbele yangu. Nilikuleteeni mbele onyo langu.
 
29Mbele yangu haibadilishwi kauli, wala Mimi siwadhulumu waja wangu.
 
30Siku tutapo iambia Jahannamu: Je! Umejaa? Nayo itasema: Je! Kuna ziada?
 
31Na Pepo italetwa karibu kwa ajili ya wachamngu, haitakuwa mbali.
 
32Haya ndiyo mnayo ahidiwa kwa kila mwenye kurejea kwa Mwenyezi Mungu na akajilinda.
 
33Mwenye kumwogopa Mwingi wa Rehema hali kuwa hamwoni, na akaja kwa moyo ulio elekea-
 
34(Ataambiwa) ingieni kwa salama. Hiyo ndiyo siku ya daima dawamu.
 
35Humo watapata wakitakacho, na kwetu yako ya ziada.
 
36Na kaumu ngapi tuliziangamiza kabla yao walio kuwa na nguvu zaidi kuliko hawa! Nao walitanga tanga katika nchi nyingi. Je! Walipata pa kukimbilia?
 
37Hakika katika hayo upo ukumbusho kwa mwenye moyo au akatega sikio naye yupo anashuhudia.
 
38Na bila ya shaka Sisi tumeziumba mbingu na ardhi na vilio baina yao mnamo siku sita; na wala hayakutugusa machofu.
 
39Basi vumilia kwa hayo wasemayo, na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa.
 
40Na katika usiku pia mtakase, na baada ya kusujudu.
 
41Na sikiliza siku atapo nadi mwenye kunadi kutoka pahala karibu.
 
42Siku watakapo sikia ukelele wa haki. Hiyo ndiyo siku ya kufufuka.
 
43Hakika Sisi tunahuisha na tunafisha, na kwetu Sisi ndio marejeo.
 
44Siku itapo wapasukia ardhi mbio mbio! Mkusanyo huo kwetu ni mwepesi.
 
45Sisi tunajua kabisa wayasemayo. Wala wewe si mwenye kuwatawalia kwa ujabari. Basi mkumbushe kwa Qur'ani anaye liogopa onyo.
 
 
ReadTheQuran.org