| Translations | Suras |
| KISWAHILI | |
44 - ADDUKHAN | |
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. | |
| 1 | H'a Mim |
| 2 | Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha, |
| 3 | Hakika tumekiteremsha katika usiku ulio barikiwa. Hakika Sisi ni Waonyaji. |
| 4 | Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikima, |
| 5 | Jambo litokalo kwetu. Hakika Sisi ndio wenye kutuma. |
| 6 | Ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia Mwenye kujua. |
| 7 | Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilio baina yao, ikiwa nyinyi mna yakini. |
| 8 | Hakuna mungu ila Yeye; anahuisha na anafisha- Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa baba zenu wa mwanzo. |
| 9 | Lakini wao wanacheza katika shaka. |
| 10 | Basi ingoje siku ambayo mbingu zitakapo leta moshi ulio dhaahiri, |
| 11 | Utakao wafunika watu: Hii ni adhabu chungu! |
| 12 | Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu hii. Hakika tutaamini. |
| 13 | Nini faida ya kukumbuka kwao? Na alikwisha wafikia Mtume mwenye kubainisha. |
| 14 | Na wao wakamgeuzia uso, na wakasema: Huyu amefunzwa, naye ni mwendawazimu. |
| 15 | Hakika sisi tutaiondoa adhabu kidogo, lakini nyinyi kwa yakini mtarejea vile vile! |
| 16 | Siku tutayo yashambulia mashambulio makubwa, bila ya shaka Sisi ni wenye kutesa. |
| 17 | Na hakika kabla ya hawa tuliwafanyia mtihani watu wa Firauni, na aliwafikia Mtume Mtukufu. |
| 18 | Akasema: Nipeni waja wa Mwenyezi Mungu; kwa hakika mimi kwenu ni Mtume Muaminifu. |
| 19 | Na msimfanyie kiburi Mwenyezi Mungu; hakika mimi nitakuleteeni uthibitisho ulio wazi. |
| 20 | Nami najikinga kwa Mola wangu Mlezi na ndiye Mola wenu Mlezi pia, ili msinipige mawe. |
| 21 | Na ikiwa hamniamini, basi jitengeni nami. |
| 22 | Ndipo akamwomba Mola wake Mlezi: Hakika watu hawa ni wakosefu. |
| 23 | Mwenyezi Mungu akasema: Basi nenda na waja wangu usiku. Kwa yakini mtafuatwa. |
| 24 | Na iache bahari vivyo hivyo imeachana, hakika wao hao ni jeshi litakalo zamishwa. |
| 25 | Mabustani mangapi, na chemchem ngapi waliziacha! |
| 26 | Na mimea na vyeo vitukufu! |
| 27 | Na neema walizo kuwa wakijistareheshea! |
| 28 | Ndio hivyo! Na tukawarithisha haya watu wenginewe. |
| 29 | La mbingu wala ardhi hazikuwalilia, wala hawakupewa muhula. |
| 30 | Na bila ya shaka tuliwaokoa Wana wa Israili katika adhabu ya kuwadhalilisha, |
| 31 | Ya Firauni. Hakika yeye alikuwa jeuri katika wenye kupindukia mipaka. |
| 32 | Na tuliwakhiari kwa ujuzi wetu kuliko walimwengu wenginewe. |
| 33 | Na tukawapa katika ishara zenye majaribio yaliyo wazi. |
| 34 | Hakika hawa wanasema: |
| 35 | Hapana ila kufa kwetu mara ya kwanza tu, wala sisi hatufufuliwi. |
| 36 | Basi warudisheni baba zetu, ikiwa nyinyi mnasema kweli. |
| 37 | Je! Ni wao bora au watu wa Tubbaa' na walio kuwa kabla yao? Tuliwaangamiza. Hakika hao walikuwa wakosefu. |
| 38 | Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake kwa mchezo. |
| 39 | Hatukuviumba hivyo ila kwa Haki, lakini wengi wao hawajui. |
| 40 | Hakika siku ya Uamuzi ni wakati ulio wekwa kwa wao wote. |
| 41 | Siku ambayo rafiki hatamfaa rafiki yake kwa chochote, wala hawatanusuriwa. |
| 42 | Isipo kuwa atakaye mrehemu Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu. |
| 43 | Hakika Mti wa Zaqqum, |
| 44 | Ni chakula cha mwenye dhambi. |
| 45 | Kama shaba iliyo yayushwa, hutokota matumboni |
| 46 | Kama kutokota kwa maji ya moto. |
| 47 | (Itasemwa:) Mkamateni na mtupeni katikati ya Jahannamu! |
| 48 | Kisha mmwagieni juu ya kichwa chake adhabu ya maji yanayo chemka. |
| 49 | Onja! Ati wewe ndiye mwenye nguvu, mtukufu! |
| 50 | Hakika haya ndiyo mliyo kuwa mkiyatilia shaka. |
| 51 | Hakika wachamngu watakuwa katika mahali pa amani, |
| 52 | Katika mabustani na chemchem, |
| 53 | Watavaa hariri nyepesi na hariri nzito wakikabiliana, |
| 54 | Hivi ndivyo itakavyo kuwa, na tutawaoza mahurilaini. |
| 55 | Humo watataka kila aina ya matunda, na wakae kwa amani. |
| 56 | Humo hawataonja mauti ila mauti yale ya kwanza, na (Mwenyezi Mungu) atawalinda na adhabu ya Jahannamu, |
| 57 | Kuwa ni fadhila zitokazo kwa Mola wako Mlezi. Huko ndiko kufuzu kukubwa. |
| 58 | Basi tumeifanya nyepesi hii Qur'ani kwa ulimi wako, ili wapate kukumbuka. |
| 59 | Ngoja tu, na wao wangoje pia. |
| ReadTheQuran.org | |