Translations Suras
KISWAHILI

36 - YA-SIN

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

 
1Ya-Sin (Y.S.).
 
2Kwa Haki ya Qur'ani yenye hikima!
 
3Hakika wewe ni miongoni mwa walio tumwa,
 
4Juu ya Njia Iliyo Nyooka.
 
5Uteremsho wa Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.
 
6Ili uwaonye watu ambao baba zao hawakuonywa , basi wao wamekuwa wenye kughafilika.
 
7Bila ya shaka kauli imekwisha thibiti juu ya wengi katika wao, kwa hivyo hawaamini.
 
8Tumeweka makongwa shingoni mwao, yakawafika videvuni. Kwa hivyo vichwa vyao viko juu tu.
 
9Tumeweka kizuizi mbele yao, na kizuizi nyuma yao, na tumewafunika macho yao; kwa hivyo hawaoni.
 
10Ni sawa sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye, hawataamini.
 
11Hakika wewe unamwonya mwenye kufuata ukumbusho, na akamcha Arrahman, Mwingi wa Rehema, kwa ghaibu. Basi mbashirie huyo msamaha na ujira mwema.
 
12Hakika Sisi tunawafufua wafu, na tunayaandika wanayo yatanguliza, na wanayo yaacha nyuma. Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari asli lenye kubainisha.
 
13Na wapigie mfano wa wakaazi wa mji walipo wafikia walio tumwa.
 
14Tulipo watumia wawili, wakawakanusha. Basi tukawazidishia nguvu kwa mwingine wa tatu. Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwenu.
 
15Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni watu kama sisi. Na Mwingi wa Rehema hakuteremsha kitu. Nyinyi mnasema uwongo tu.
 
16Wakasema: Mola wetu Mlezi anajua kwamba hakika sisi tumetumwa kwenu.
 
17Wala si juu yetu ila kufikisha ujumbe ulio wazi.
 
18Wakasema: Sisi tumeagua kuwa nyinyi ni wakorofi. Ikiwa hamtaacha basi kwa yakini tutakupigeni mawe, na mtapata adhabu chungu kutoka kwetu.
 
19Wakasema: Ukorofi wenu mnao wenyewe! Je! Ni kwa kuwa mnakumbushwa? Ama nyinyi ni watu walio pindukia mipaka.
 
20Na akaja mtu mbio kutokea upande wa mbali wa mjini, akasema: Enyi watu wangu! Wafuateni hawa walio tumwa.
 
21Wafuateni ambao hawakutakini ujira, hali ya kuwa wenyewe wameongoka.
 
22NA KWA NINI nisimuabudu yule aliye niumba na kwake mtarejeshwa?
 
23Je! Niishike miungu mingine badala yake? Arrahmani, Mwingi wa Rehema, akinitakia madhara uombezi wa hao hautanifaa kitu, wala hawataniokoa.
 
24Basi hakika mimi hapo nitakuwa katika upotovu ulio dhaahiri.
 
25Hakika mimi nimemuamini Mola wenu Mlezi, basi nisikilizeni!
 
26Akaambiwa: Ingia Peponi! Akasema: Laiti kuwa watu wangu wangeli jua
 
27Jinsi Mola wangu Mlezi alivyo nisamehe, na akanifanya miongoni mwa walio hishimiwa.
 
28Na hatukuwateremshia kaumu yake baada yake jeshi kutoka mbinguni, wala si wenye kuteremsha.
 
29Hakukuwa ila ukelele mmoja tu; na mara walizimwa!
 
30Nawasikitikia waja wangu. Hawajii Mtume ila wao humkejeli.
 
31Je! Hawaoni umma ngapi tulizo ziangamiza kabla yao? Hakika hao hawarejei tena kwao.
 
32Na hapana mmoja ila wote watakusanywa waletwe mbele yetu.
 
33Na Ishara hiyo kwao - ardhi iliyo kufa, nasi tukaifufua, na tukatoa ndani yake nafaka, wakawa wanazila!
 
34Na tukafanya ndani yake mabustani ya mitende na mizabibu, na tukatimbua chemchem ndani yake,
 
35Ili wale matunda yake, na hayo hayakufanywa na mikono yao! Basi je, hawashukuru?
 
36Subhana, Ametakasika, aliye umba dume na jike vyote katika vinavyo mea katika ardhi na katika nafsi zao, na katika wasivyo vijua.
 
37Na usiku ni Ishara kwao. Tunauvua humo mchana, mara wao wanakuwa gizani.
 
38Na jua linakwenda kwa kiwango chake. Hayo ni makadirio ya Mwenye nguvu, Mwenye kujua.
 
39Na mwezi tumeupimia vituo, mpaka unakuwa kama karara kongwe.
 
40Haliwi jua kuufikia mwezi, wala usiku kuupita mchana. Na vyote vinaogelea katika njia zao.
 
41Na ni Ishara kwao kwamba Sisi tuliwapakia dhuriya zao katika jahazi ilio sheheni.
 
42Na tukawaumbia kutoka mfano wake wanavyo vipanda.
 
43Na tukitaka tunawazamisha, wala hapana wa kuwasaidia, wala hawaokolewi,
 
44Isipo kuwa kwa rehema zitokazo kwetu na starehe kwa muda.
 
45Na wanapo ambiwa: Jilindeni na yalioko mbele yenu na yalioko nyuma yenu, ili mpate kurehemewa...
 
46Na haiwafikii Ishara yoyote katika Ishara za Mola wao Mlezi ila wao huwa ni wenye kuipuuza.
 
47Na wanapo ambiwa: Toeni katika aliyo kupeni Mwenyezi Mungu, walio kufuru huwaambia walio amini: Je! Tuwalishe ambao Mwenyezi Mungu angependa angeli walisha mwenyewe? Nyinyi hammo ila katika upotofu ulio dhaahiri.
 
48Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi ni wakweli?
 
49Hawangojei ila ukelele mmoja tu utakao wachukua nao wamo kuzozana.
 
50Basi hawataweza kuusia, wala kwa watu wao hawarejei.
 
51Na litapulizwa barugumu, mara watatoka makaburini wakikimbilia kwa Mola wao Mlezi.
 
52Watasema: Ole wetu! Nani aliye tufufua kwenye malazi yetu? Haya ndiyo aliyo yaahidi Mwingi wa Rehema na wakasema kweli Mitume.
 
53Haitakuwa ila ukelele mmoja tu, mara wote watahudhuruishwa mbele yetu.
 
54Basi leo nafsi yoyote haitadhulumiwa kitu, wala hamtalipwa ila yale mliyo kuwa mkiyatenda.
 
55Hakika watu wa Peponi leo wamo shughulini, wamefurahi.
 
56Wao na wake zao wamo katika vivuli wameegemea juu ya viti vya fakhari.
 
57Watapata humo kila namna ya matunda na watapata kila watakacho kitaka.
 
58"Salama!" Hiyo ndiyo kauli itokayo kwa Mola Mlezi Mwenye kurehemu.
 
59Na enyi wakosefu! Jitengeni leo!
 
60Je! Sikuagana nanyi, enyi wanaadamu, kuwa msimuabudu Shet'ani? Hakika yeye ni adui dhaahiri kwenu.
 
61Na ya kwamba mniabudu Mimi? Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.
 
62Na bila ya shaka yeye amekwisha lipoteza kundi kubwa miongoni mwenu. Je, hamkuwa mkifikiri?
 
63Hii basi ndiyo Jahannamu mliyo kuwa mkiahidiwa.
 
64Ingieni leo kwa vile mlivyo kuwa mkikufuru.
 
65Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyachuma.
 
66Na tungeli penda tungeli yafutilia mbali macho yao, wakawa wanaiwania njia. Lakini wange ionaje?
 
67Na tungeli taka tunge wageuza sura hapo hapo walipo, basi wasinge weza kwenda wala kurudi.
 
68Na tunaye mzeesha tunamrudisha nyuma katika umbo. Basi je! hawazingatii?
 
69Wala hatukumfundisha (Muhammad) mashairi, wala hayatakikani kwake hayo. Haukuwa huu ila ni ukumbusho na Qur'ani inayo bainisha.
 
70Ili imwonye aliye hai, na neno litimie juu ya makafiri.
 
71Je! Hawaoni kwamba tumewaumbia kutokana na iliyo fanya mikono yetu wanyama wa mifugo, na wao wakawa wenye kuwamiliki.
 
72Na Sisi tukawadhalilishia. Basi baadhi yao wako wanao wapanda, na baadhi yao wanawala.
 
73Na wao wanapata kwao manufaa na vinywaji. Basi je, hawashukuru?
 
74Na wameishika miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu ili ati wapate kusaidiwa!
 
75Hawataweza kuwasaidia. Bali hao ndio watakuwa askari wao watakao hudhurishwa.
 
76Basi maneno yao yasikuhuzunishe. Hakika Sisi tunayajua wanayo yaweka siri na wanayo yatangaza.
 
77Kwani mwanaadamu haoni ya kwamba Sisi tumemuumba yeye kutokana na tone la manii? Kisha sasa yeye ndio amekuwa ndiye mgomvi wa dhaahiri!
 
78Na akatupigia mfano, na akasahau kuumbwa kwake, akasema: Ni nani huyo atakaye ihuisha mifupa nayo imekwisha mung'unyika?
 
79Sema: Ataihuisha huyo huyo aliye iumba hapo mara ya mwanzo. Na Yeye ni Mjuzi wa kila kuumba.
 
80Aliye kujaalieni kupata moto kutokana na mti wa kijani nanyi mkawa kwa huo mnawasha.
 
81Kwani aliye ziumba mbingu na ardhi hawezi kuwaumba mfano wao? Kwani! Naye ndiye Muumbaji Mkuu, Mjuzi.
 
82Hakika amri yake anapo taka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kikawa.
 
83Basi Ametakasika yule ambaye mkononi mwake umo Ufalme wa kila kitu; na kwake Yeye mtarejeshwa.
 
 
ReadTheQuran.org