Translations Suras
KISWAHILI

34 - SABAA

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

 
1Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, ambaye ni vyake vyote viliomo mbnguni na katika ardhi. Na sifa ni zake Yeye katika Akhera. Naye ni Mwenye hikima, Mwenye khabari.
 
2Anajua yanayo ingia katika ardhi na yanayo toka humo, na yanayo teremka kutoka mbinguni, na yanayo panda huko. Na Yeye ni Mwenye kurehemu, Mwenye kusamehe.
 
3Na walisema walio kufuru: Haitatufikia Saa (ya Kiyama). Sema: Kwani? Hapana shaka itakufikieni, naapa kwa haki ya Mola wangu Mlezi, Mwenye kujua ya ghaibu! Hapana kinacho fichikana kwake hata chenye uzito wa chembe tu, si katika mbingu wala katika ardhi, wala kilicho kidogo kuliko hivyo, wala kikubwa zaidi; ila vyote hivyo vimo katika Kitabu chake chenye kubainisha.
 
4Ili awalipe walio amini na wakatenda mema. Hao watapata msamaha na riziki ya ukarimu.
 
5Na wale walio jitahidi kuzipinga Ishara zetu wakaona watashinda, hao watapata adhabu mbaya yenye uchungu.
 
6Na walio pewa ilimu wanaona ya kuwa ulio teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi ni haki, nayo huongoa kwendea njia ya Mwenye nguvu, Mwenye kusifiwa.
 
7Na walio kufuru walisema: Je! Tukujuulisheni mtu anaye kuambieni kwamba mtakapo chambuliwa mapande mapande mtakuwa katika umbo jipya?
 
8Ama amemzulia Mwenyezi Mungu uwongo, au ana wazimu. Bali wasio amini Akhera wamo adhabuni na upotofu wa mbali kabisa.
 
9Kwani hawaoni yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao ya mbingu na ardhi? Tungeli penda tungeli wadidimiza ndani ya ardhi, au tungeli wateremshia juu yao vipande vya mbingu. Hakika katika haya zipo Ishara kwa kila mja aliye tubia.
 
10Na tulimpa Daudi fadhila kutoka kwetu, (tukasema): Enyi milima! Karirini kumtakasa Mwenyezi Mungu pamoja naye! Na ndege pia. Na tukamlainishia chuma.
 
11(Tukamwambia:) Tengeneza nguo za chuma pana, na kadiria sawa katika kuunganisha. Na tendeni mema. Hakika Mimi nayaona vyema mnayo yatenda.
 
12Na Suleiman tuliufanya upepo umtumikie. Safari yake ya asubuhi ni mwendo wa mwezi mmoja, na safari yake ya jioni ni mwendo wa mwezi mmoja. Na tukamyayushia chemchem ya shaba. Na katika majini walikuwako walio kuwa wakifanya kazi mbele yake kwa idhini ya Mola wake Mlezi. Na kila anaye jitenga na amri yetu katika wao, tunamwonjesha adhabu ya Moto unao waka.
 
13Walikuwa wakimfanyia alipendalo, kama mihrabu, na masanamu, na madeste makubwa kama mahodhi, na masufuria makubwa yasiyo ondolewa mahala pake. Enyi watu wa Daudi! Fanyeni kazi kwa kushukuru. Ni wachache katika waja wangu wanao shukuru.
 
14Na tulipo mhukumia kufa, hapana aliye wajuulisha kufa kwake ila mnyama wa ardhi aliye kula fimbo yake. Na alipo anguka majini walitambua lau kuwa wangeli jua ya ghaibu wasingeli kaa katika adhabu hiyo ya kufedhehesha.
 
15Hakika ilikuwapo Ishara kwa (watu wa nchi ya) Sabaa katika maskani yao - bustani mbili, kulia na kushoto. Kuleni katika riziki ya Mwenyezi Mungu, na mumshukuru. Mji mzuri na Mola Mlezi aliye Msamehevu.
 
16Lakini wakaacha. Tukawapelekea mafuriko makubwa, na tukawabadilishia badala ya bustani zao hizo kwa bustani nyengine zenye matunda makali machungu, na mivinje, na kidogo katika miti ya kunazi.
 
17Hayo tuliwalipa kwa sababu ya walivyo kufuru. Nasi kwani tunamuadhibu isipo kuwa anaye kufuru?
 
18Na baina yao na miji mingine tuliyo ibariki tuliweka miji iliyo dhaahiri, na tukaweka humo vituo vya safari. Tukawaambia: Nendeni humo usiku na mchana kwa amani.
 
19Lakini wakasema: Mola wetu Mlezi! Weka mwendo mrefu baina ya safari zetu. Na wakazidhulumu nafsi zao. Basi tukawafanya ni masimulizi tu, na tukawatawanya tawanya. Hakika katika hayo bila ya shaka zimo Ishara kwa kila mwenye kusubiri sana na akashukuru.
 
20Na bila ya shaka Iblisi alihakikisha ile dhana yake juu yao. Nao walimfuata, isipo kuwa kundi la Waumini.
 
21Na yeye hakuwa na mamlaka yoyote juu yao, ila kwa sababu ya kuwajaribu tujue nani mwenye kuamini Akhera, na nani anaye tilia shaka. Na Mola wako Mlezi ni Mwenye kuhifadhi kila kitu.
 
22Sema: Waite mnao wadaia kuwa ni badala ya Mwenyezi Mungu. Hawamiliki hata uzito wa chembe hichi katika mbingu wala ardhi. Wala hawana ushirika wowote humo. Wala Yeye hana msaidizi miongoni mwao.
 
23Wala uombezi mbele yake hautafaa kitu, isipo kuwa kwa aliye mpa idhini. Hata itapo ondolewa khofu kwenye nyoyo zao watasema: Mola wenu Mlezi kasema nini? Watasema: Yaliyo kweli! Na Yeye ndiye Aliye juu, Mkubwa.
 
24Sema: Ni nani anaye kuruzukuni kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Sema: Mwenyezi Mungu! Na hakika sisi au nyinyi bila ya shaka tuko kwenye uwongofu au upotofu ulio wazi.
 
25Sema: Nyinyi hamtaulizwa kwa makosa tuliyo yafanya, wala sisi hatutaulizwa kwa mnayo yatenda nyinyi.
 
26Sema: Mola wetu Mlezi atatukusanya, kisha atatuhukumu kwa haki; na Yeye ndiye Hakimu Mwenye kujua.
 
27Sema: Nionyesheni mlio waunganisha naye kuwa washirika. Hasha! Bali Yeye ndiye Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
 
28Na hatukukutuma ila kwa watu wote, uwe mbashiri, na mwonyaji. Lakini watu wengi hawajui.
 
29Na wanasema: Ahadi hii itakuwa lini, ikiwa nyinyi mnasema kweli?
 
30Sema: Nyinyi mnayo miadi ya Siku ambayo hamtaakhirika nayo kwa saa moja, wala hamtaitangulia.
 
31Na walisema walio kufuru: Hatutaiamini Qur'ani hii, wala yaliyo kuwa kabla yake. Na ungeli waona madhaalimu watapo simamishwa mbele ya Mola wao Mlezi, wakirudishiana maneno wao kwa wao! Wanyonge wakiwaambia walio takabari: Lau kuwa si nyinyi, bila ya shaka tungeli kuwa Waumini sisi.
 
32Walio takabari watawaambia wanyonge: Kwani sisi ndio tulio kuzuieni na uwongofu baada ya kukujieni? Bali nyinyi wenyewe ni wakosefu.
 
33Na wanyonge wakawaambia walio takabari: Bali ni vitimbi vyenu vya usiku na mchana, mlipo kuwa mkituamrisha tumkufuru Mwenyezi Mungu, na tumfanyie washirika. Nao wataficha majuto watakapo iona adhabu. Na tutaweka makongwa shingoni mwao walio kufuru. Kwani wanalipwa ila kwa waliyo kuwa wakiyatenda?
 
34Na hatukumtuma mwonyaji yeyote kwenye mji, ila walisema walio jidekeza kwa starehe zao wa mji huo: Hakika sisi tunayakataa hayo mliyo tumwa nayo.
 
35Na wakasema: Sisi tuna mali mengi zaidi na watoto, wala sisi hatutaadhibiwa.
 
36Sema: Hakika Mola wangu Mlezi humkunjulia riziki na humdhikisha amtakaye. Lakini watu wengi hawajui.
 
37Na si mali yenu wala watoto wenu watakao kukaribisheni kwetu muwe karibu, isipo kuwa aliye amini na akatenda mema. Hao basi watapata malipo mardufu kwa walio yafanya. Nao watakuwa salama katika maghorofa.
 
38Na wanao jitahidi kuzipinga Ishara zetu, wakaona watashinda, hao watahudhurishwa kwenye adhabu.
 
39Sema: Kwa hakika Mola wangu Mlezi humkunjulia riziki na humdhikisha amtakaye katika waja wake. Na chochote mtakacho kitoa Yeye atakilipa. Naye ni Mbora wa wanao ruzuku.
 
40Na siku atakayo wakusanya wote, kisha atawaambia Malaika: Je! Hawa walikuwa wakikuabuduni?
 
41Waseme: Subhanak, Umetakasika. Wewe ndiye kipenzi chetu si hao. Bali wao walikuwa wakiwaabudu majini; wengi wao wakiwaamini hao.
 
42Hii leo hataweza yeyote kumletea nafuu wala madhara mwenzie. Na tutawaambia walio dhulumu: Onjeni adhabu ya Moto mlio kuwa mkiukanusha.
 
43Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi wanasema: Huyu si chochote ila ni mtu anaye taka kukuzuieni na waliyo kuwa wakiabudu baba zenu. Na wakasema: Haya si chochote ila ni uwongo ulio zuliwa. Na walio kufuru waliiambia Haki ilipo wajia: Haya si chochote ila ni uchawi ulio dhaahiri.
 
44Wala hatukuwapa Vitabu wavisome, wala hatukuwatumia Mwonyaji kabla yako wewe.
 
45Na walikadhibisha walio kuwa kabla yao. Na hawakufikilia hata sehemu moja katika kumi ya tulivyo wapa hao. Nao waliwakadhibisha Mitume wangu. Basi kuangamiza kwangu kulikuwa namna gani!
 
46Sema: Mimi nakunasihini kwa jambo moja tu - ya kwamba msimame kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wawili-wawili na mmoja-mmoja; kisha mfikiri. Mwenzenu huyu hana wazimu. Yeye si chochote ila ni Mwonyaji kwenu kabla ya kufika adhabu kali.
 
47Sema: Ujira nilio kuombeni ni wenu nyinyi. Sina ujira ila kwa Mwenyezi Mungu. Na Yeye ni Shahidi juu ya kila kitu.
 
48Sema: Hakika Mola wangu Mlezi anaondoa upotovu kwa Haki. Yeye ndiye Mwenye kujua vyema yaliyo ghaibu.
 
49Sema: Kweli imefika, na uwongo haujitokezi, wala haurudi.
 
50Sema: Ikiwa mimi nimepotea, basi nimepotea kwa kudhuru nafsi yangu mwenyewe. Na ikiwa nimeongoka, basi ni kwa sababu ya kunifunulia Mola wangu Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Aliye karibu.
 
51Na lau ungeli ona watapo babaika, basi hapana pa kukimbilia! Na watakamatwa mahala pa karibu.
 
52Na watasema: Tunaiamini! Lakini wataipata wapi kutoka huko mahala mbali?
 
53Na hapo kabla yake waliikataa, na wakiyatupilia mbali maneno ya ghaibu kutoka mahali mbali.
 
54Na watatiliwa kizuizi baina yao na hayo wanayo yatamani, kama walivyo fanyiwa wenzao zamani. Hakika hao walikuwa na shaka ya kutia wasiwasi.
 
 
ReadTheQuran.org