Translations Suras
KISWAHILI

26 - ASH-SHUA'RAA

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

 
1T'aa Siin Miim. (T'.S.M.)
 
2Hizi ni Aya za Kitabu kinacho bainisha.
 
3Huenda labda ukajikera nafsi yako kwa kuwa hawawi Waumini.
 
4Tunge penda tungeli wateremshia kutoka mbinguni Ishara zikanyenyekea shingo zao.
 
5Wala hauwafikii ukumbusho mpya kutoka kwa Arrahman ila wao hujitenga nao.
 
6Kwa yakini wamekanusha; kwa hivyo zitakuja wafikia khabari za yale waliyo kuwa wakiyafanyia mzaha.
 
7Je! Hawakuiona ardhi, mimea mingapi tumeiotesha humo, ya kila namna nzuri?
 
8Hakika katika haya zipo Ishara. Lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.
 
9Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
 
10Na Mola wako Mlezi, alipo mwita Musa, akamwambia: Fika kwa watu madhaalimu,
 
11Watu wa Firauni. Hawaogopi?
 
12Akasema: Hakika mimi nachelea wasinikanushe.
 
13Na kifua changu kina dhiki, na ulimi wangu haukunjuki vyema. Basi mtumie ujumbe Harun.
 
14Na wao wana kisasi juu yangu, kwa hivyo naogopa wasije kuniuwa.
 
15Akasema: Siyo hivyo kabisa! Nendeni na miujiza yetu. Hakika Sisi tu pamoja nanyi, tunasikiliza.
 
16Basi mfikieni Firauni na mwambieni: Hakika sisi ni Mitume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
 
17Waachilie Wana wa Israili wende nasi.
 
18(Firauni) akasema: Sisi hatukukulea wewe utotoni, na ukakaa kwetu katika umri wako miaka mingi?
 
19Na ukatenda kitendo chako ulicho tenda, nawe ukawa miongoni mwa wasio na shukrani?
 
20(Musa) akasema: Nilitenda hayo hapo nilipo kuwa miongoni mwa wale walio potea.
 
21Basi nikakukimbieni nilipo kuogopeni, tena Mola wangu Mlezi akanitunukia hukumu, na akanijaalia niwe miongoni mwa Mitume.
 
22Na hiyo ndiyo neema ya kunisumbulia, na wewe umewatia utumwani Wana wa Israili?
 
23Firauni akasema: Na nani huyo Mola Mlezi wa walimwengu wote?
 
24Akasema: Ndiye Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi ni wenye yakini.
 
25(Firauni) akawaambia walio mzunguka: Hamsikilizi?
 
26(Musa) akasema: Ndiye Mola wenu Mlezi, na Mola Mlezi wa baba zenu wa kwanza.
 
27(Firauni) akasema: Hakika huyu Mtume wenu aliye tumwa kwenu ni mwendawazimu.
 
28(Musa) akasema: Ndiye Mola Mlezi wa Mashariki na Magharibi na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi mnatia akilini.
 
29(Firauni) akasema: Ukimfuata mungu mwengine asiye kuwa mimi, basi bila ya shaka nitakufunga gerezani.
 
30Akasema: Je! Ijapo kuwa nitakuletea kitu cha kubainisha wazi?
 
31Akasema: Kilete basi, kama wewe ni katika wasemao kweli.
 
32Basi akaitupa fimbo yake, mara ikawa nyoka wa kuonekana dhaahiri.
 
33Na akautoa mkono wake, na mara ukawa mweupe kwa watazamao.
 
34(Firauni) akawaambia waheshimiwa walio mzunguka: Hakika huyu ni mchawi mtaalamu.
 
35Anataka kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wake. Basi mna shauri gani?
 
36Wakasema: Mpe muda yeye na nduguye na uwatume mijini wapigao mbiu ya mgambo.
 
37Wakuletee kila mchawi bingwa mtaalamu.
 
38Basi wakakusanywa wachawi wakati na siku maalumu.
 
39Na watu wakaambiwa: Je! Mtakusanyika?
 
40Huenda tutawafuata wachawi wakiwa wao ndio watakao shinda.
 
41Basi walipo kuja wachawi wakamwambia Firauni: Je! Tutapata ujira tukiwa sisi ndio tulio shinda?
 
42Naam! Na hakika mtakuwa katika watu wa mbele.
 
43Musa akwaambia: Tupeni mnavyo taka kutupa.
 
44Basi wakatupa kamba zao na fimbo zao, na wakasema: Kwa nguvu za Firauni hakika sisi hapana shaka ni wenye kushinda.
 
45Musa tena akatupa fimbo yake, nayo mara ikavimeza walivyo vizua.
 
46Hapo wachawi walipinduka wakasujudu.
 
47Wakasema: Tunamuamini Mola Mlezi wa walimwengu wote.
 
48Mola Mlezi wa Musa na Harun.
 
49(Firauni) akasema: Je! Mmemuamini kabla sijakuruhusuni? Bila ya shaka yeye basi ndiye mkubwa wenu aliye kufunzeni uchawi. Basi mtakuja jua! Nitakata mikono yenu na miguu yenu kwa kutafautisha. Na nitakubandikeni misalabani nyote.
 
50Wakasema: Haidhuru, kwani sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi.
 
51Hakika sisi tunatumai Mola wetu Mlezi atatusamehe makosa yetu, kwa kuwa ndio wa kwanza wa kuamini.
 
52Na tulimuamrisha Musa kwa wahyi: Nenda na waja wangu wakati wa usiku. Kwa hakika mtafuatwa.
 
53Basi Firauni akawatuma mijini wapiga mbiu za mgambo.
 
54(Wakieneza): Hakika hawa ni kikundi kidogo.
 
55Nao wanatuudhi.
 
56Na sisi ni wengi, wenye kuchukua hadhari.
 
57Basi tukawatoa katika mabustani na chemchem,
 
58Na makhazina, na vyeo vya hishima,
 
59Kadhaalika; na tukawarithisha hayo Wana wa Israili.
 
60Basi wakawafuata lilipo chomoza jua.
 
61Na yalipo onana majeshi mawili haya, watuwa Musa wakasema: Hakika sisi bila ya shaka tumepatikana!
 
62(Musa) akasema: Hasha! Hakika yu pamoja nami Mola wangu Mlezi. Yeye ataniongoa!
 
63Tulimletea wahyi Musa tukamwambia: Piga bahari kwa fimbo yako. Basi ikatengana, na kila sehemu ikawa kama mlima mkubwa.
 
64Na tukawajongeza hapo wale wengine.
 
65Tukawaokoa Musa na walio kuwa pamoja naye wote.
 
66Kisha tukawazamisha hao wengine.
 
67Hakika bila ya shaka katika hayo ipo Ishara; lakini wengi wao si katika wenye kuamini.
 
68Na kwa hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
 
69Na wasomee khabari za Ibrahim.
 
70Alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Mnaabudu nini?
 
71Wakasema: Tunaabudu masanamu, daima tunayanyenyekea.
 
72Akasema: Je! Yanakusikieni mnapo yaita?
 
73Au yanakufaeni, au yanakudhuruni?
 
74Wakasema: Bali tumewakuta baba zetu wakifanya hivyo hivyo.
 
75Je! Mmewaona hawa mnao waabudu-
 
76Nyinyi na baba zenu wa zamani?
 
77Kwani hakika hao ni adui zangu, isipo kuwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
 
78Ambaye ndiye aliye niumba, na Yeye ndiye ananiongoa,
 
79Na ambaye ndiye ananilisha na kuninywesha.
 
80Na ninapo ugua ni Yeye ndiye anaye niponesha.
 
81Na ambaye atanifisha, na kisha atanihuisha.
 
82Na ambaye ndiye ninaye mtumai kunisamehe makosa yangu Siku ya Malipo.
 
8383, Mola wangu Mlezi! Nitunukie hukumu na uniunganishe na watendao mema.
 
84Na unijaalie nitajwe kwa wema na watu watakao kuja baadaye.
 
85Na unijaalie katika warithi wa Bustani za neema.
 
86Na umsamehe baba yangu, kwani hakika alikuwa miongoni mwa wapotovu.
 
87Wala usinihizi Siku watapo fufuliwa.
 
88Siku ambayo kwamba mali hayato faa kitu wala wana.
 
89Isipo kuwa mwenye kumjia Mwenyezi Mungu na moyo safi.
 
90Na Pepo itasogezwa kwa wachamngu.
 
91Na Jahannamu itadhihirishwa kwa wapotovu.
 
92Na wataambiwa: Wako wapi mlio kuwa mkiwaabudu
 
93Badala ya Mwenyezi Mungu? Je! Wanakusaidieni, au wanajisaidia wenyewe?
 
94Basi watavurumizwa humo wao na hao wakosefu,
 
95Na majeshi ya Ibilisi yote.
 
96Watasema, na hali ya kuwa wanazozana humo:
 
97Wallahi! Kwa yakini tulikuwa katika upotovu ulio dhaahiri,
 
98Tulipo kufanyeni ni sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote.
 
99Na hawakutupoteza ila wale wakosefu.
 
100Basi hatuna waombezi.
 
101Wala rafiki wa dhati.
 
102Laiti tungeli pata kurejea tena tungeli kuwa katika Waumini.
 
103Hakika katika haya ipo Ishara, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.
 
104Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
 
105Kaumu ya Nuhu waliwakadhibisha Mitume.
 
106Alipo waambia ndugu yao, Nuhu: Je! Hamchimngu?
 
107Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.
 
108Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi.
 
109Na sikutakini juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
 
110Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi.
 
111Wakasema: Je! Tukuamini wewe, hali wanao kufuata ni watu wa chini?
 
112Akasema: Nayajuaje waliyo kuwa wakiyafanya?
 
113Hisabu yao haiko ila kwa Mola wao Mlezi, laiti mngeli tambua!
 
114Wala mimi si wa kuwafukuza Waumini.
 
115Mimi si cho chote ila ni Mwonyaji wa dhaahiri shaahiri.
 
116Wakasema: Ikiwa huachi, ewe Nuhu, bila ya shaka utapigwa mawe.
 
117Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wamenikanusha.
 
118Basi hukumu baina yangu na wao kwa hukumu yako, na uniokoe mimi na walio pamoja nami, Waumini.
 
119Kwa hivyo tukamwokoa yeye na walio kuwa pamoja naye katika marikebu iliyo sheheni.
 
120Kisha tukawazamisha baadaye walio bakia.
 
121Hakika katika haya ipo Ishara, lakini si wengi wao walio kuwa Waumini.
 
122Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
 
123Kina A'd waliwakanusha Mitume.
 
124Alipo waambia ndugu yao, Hud: Je! Hamchimngu?
 
125Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.
 
126Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi.
 
127Wala sikutakeni juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
 
128Je! Mnajenga juu ya kila mnyanyuko kumbusho la kufanyia upuuzi?
 
129Na mnajenga majengo ya fakhari kama kwamba mtaishi milele!
 
130Na mnapo tumia nguvu mnatumia nguvu kwa ujabari.
 
131Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini.
 
132Na mcheni aliye kupeni haya mnayo yajua.
 
133Amekupeni wanyama wa kufuga na wana.
 
134Na mabustani na chemchem.
 
135Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya Siku Kubwa.
 
136Wakasema: Ni mamoja kwetu, ukitupa mawaidha au hukuwa miongoni mwa watoao mawaidha.
 
137Haya si chochote ila ni mtindo wa watu wa tokea zamani.
 
138Wala sisi hatutaadhibiwa.
 
139Wakamkanusha; nasi tukawaangamiza. Hakika bila ya shaka katika haya ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
 
140Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
 
141Kina Thamud waliwakanusha Mitume.
 
142Alipo waambia ndugu yao Saleh: Je! Hamumchimngu?
 
143Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.
 
144Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini.
 
145Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
 
146Je! Mtaachwa salama usalimina katika haya yaliyopo hapa?
 
147Katika mabustani, na chemchem?
 
148Na konde na mitende yenye makole yaliyo wiva.
 
149Na mnachonga milimani majumba kwa ustadi.
 
150Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi.
 
151151, Wala msit'ii amri za walio pindukia mipaka,
 
152Ambao wanafanya ufisadi katika nchi, wala hawatengenezi.
 
153Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa walio rogwa.
 
154Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi. Basi lete Ishara ukiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.
 
155Akasema: Huyu ngamia jike; awe na zamu yake ya kunywa, na nyinyi muwe na zamu yenu ya kunywa katika siku maalumu.
 
156Wala msimguse kwa uwovu, isije ikakushikeni adhabu ya Siku Kubwa.
 
157Lakini wakamuuwa, na wakawa wenye kujuta.
 
158Basi ikawapata adhabu. Hakika katika hayo ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
 
159Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
 
160Watu wa Lut'i waliwakanusha Mitume.
 
161Alipo waambia ndugu yao, Lut'i: Je! Hamumchimngu?
 
162Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu kwenu.
 
163Basi mcheni Mwenyezi Mungu na nit'iini mimi.
 
164Wala mimi sikutakini ujira juu yake; ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
 
165Je! Katika viumbe vyote mnawaingilia wanaume?
 
166Na mnaacha alicho kuumbieni Mola wenu Mlezi katika wake zenu? Ama kweli nyinyi ni watu mnao ruka mipaka!
 
167Wakasema: Ewe Lut'i! Usipo acha, hapana shaka utakuwa miongoni mwa wanao tolewa mji!
 
168Akasema: Hakika mimi ni katika wanao kichukia hichi kitendo chenu.
 
169Mola wangu Mlezi! Niokoe mimi na ahali zangu na haya wayatendayo.
 
170Basi tukamwokoa yeye na ahali zake wote,
 
171Isipo kuwa kikongwe katika walio kaa nyuma.
 
172Kisha tukawaangamiza wale wengine.
 
173Na tukawanyeshea mvua, basi ni ovu mno mvua ya waliyo onywa.
 
174Hakika katika hayo ipo Ishara. Na hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
 
175Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.
 
176Watu wa Machakani waliwakanusha Mitume.
 
177Shuaibu alipo waambia: Je! Hamfanyi mkamchamngu?
 
178Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.
 
179Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi.
 
180Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
 
181Timizeni kipimo sawa sawa, wala msiwe katika wanao punja.
 
182Na pimeni kwa haki iliyo nyooka;
 
183Wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye jeuri kwa ufisadi.
 
184Na mcheni aliye kuumbeni nyinyi na vizazi vilivyo tangulia.
 
185Wakasema: Hakika wewe ni katika walio rogwa.
 
186Na wewe si chochote ila ni mtu tu kama sisi, na kwa yakini tunakuona wewe ni katika waongo.
 
187Hebu tuangushie vipande kutoka mbinguni ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.
 
188Akasema: Mola wangu Mlezi anajua zaidi mnayo yatenda.
 
189Basi walimkanusha, na ikawashika adhabu ya siku ya kivuli. Hakika hiyo ilikuwa adhabu ya siku kubwa.
 
190Hakika katika hayo ipo Ishara, lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
 
191Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
 
192Na bila ya shaka hii ni Uteremsho wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
 
193Ameuteremsha Roho muaminifu,
 
194Juu ya moyo wako, ili uwe katika Waonyaji,
 
195Kwa ulimi wa Kiarabu ulio wazi.
 
196Na hakika bila ya shaka haya yamo katika Vitabu vya kale.
 
197Je! Haikuwa kwao ni Ishara kwamba wanayajua haya wanazuoni wa Wana wa Israili?
 
198Na lau kuwa tungeli iteremsha juu ya mmoja wa wasio kuwa Waarabu,
 
199Na akawasomea, wasingeli kuwa wenye kuamini.
 
200Namna hivi tunaingiza katika nyoyo za wakosefu.
 
201Hawataiamini mpaka waione adhabu chungu.
 
202Basi itawafikia kwa ghafla, na hali hawana khabari.
 
203Na watasema: Je, tutapewa muhula?
 
204Basi, je, wanaihimiza adhabu yetu?
 
205Waonaje kama tukiwastarehesha kwa miaka,
 
206Kisha yakawafikia waliyo kuwa wakiahidiwa,
 
207Yatawafaa nini yale waliyo stareheshewa?
 
208Wala hatukuangamiza mji wo wote ila ulikuwa na waonyaji -
 
209Kuwa ni ukumbusho. Wala Sisi hatukuwa wenye kudhulumu.
 
210Wala Mashet'ani hawakuteremka nayo,
 
211Wala haitakiwi kwao, na wala hawawezi.
 
212Hakika hao wametengwa na kusikia.
 
213Basi usimwombe mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu ukawa miongoni mwa watakao adhibiwa.
 
214Na uwaonye jamaa zako walio karibu nawe.
 
215Na watwae kwa upole wanao kufuata miongoni mwa Waumini.
 
216Na ikiwa watakuasi basi sema: Mimi najitenga mbali na hayo mnayo yatenda.
 
217Na umtegemee Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
 
218Ambaye anakuona unapo simama,
 
219Na mageuko yako kati ya wanao sujudu.
 
220Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua.
 
221Je! Nikwambieni nani wanawashukia Mashet'ani?
 
222Wanamshukia kila mzushi mkubwa mwingi wa dhambi.
 
223Wanawapelekea yale wanayo yasikia; na wengi wao ni waongo.
 
224Na watungaji mashairi ni wapotofu ndio wanawafuata.
 
225Je! Huwaoni kwamba wao wanatangatanga katika kila bonde?
 
226Na kwamba wao husema wasiyo yatenda?
 
227Isipo kuwa wale walio amini, na wakatenda mema, na wakamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi, na wakajitetea wanapo dhulumiwa. Na wanao dhulumu watakuja jua mgeuko gani watakao geuka.
 
 
ReadTheQuran.org