Translations Suras
KISWAHILI

23 - AL - MUUMINUN

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

 
1HAKIKA wamefanikiwa Waumini,
 
2Ambao ni wanyenyekevu katika Sala zao,
 
3Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi,
 
4Na ambao wanatoa Zaka,
 
5Na ambao wanazilinda tupu zao,
 
6Isipo kuwa kwa wake zao au kwa iliyo wamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa.
 
7Lakini anaye taka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka.
 
8Na ambao wanazitimiza amana zao na ahadi zao,
 
9Na ambao Sala zao wanazihifadhi -
 
10Hao ndio warithi,
 
11Ambao watairithi Pepo ya Firdausi, wadumu humo.
 
12Na kwa yakini tumemuumba mtu kutokana na asli ya udongo.
 
13Kisha tukamjaalia awe tone ya mbegu ya uzazi katika kalio madhubuti.
 
14Kisha tukaiumba tone kuwa damu iliyo ganda, na tukaiumba damu kuwa pande la nyama, kisha tukaliumba pande la nyama kuwa mifupa, na mifupa tukaivika nyama. Kisha tukamfanya kiumbe mwengine. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu Mbora wa waumbaji.
 
15Kisha hakika nyinyi baada ya hayo mtakufa.
 
16Kisha hakika nyinyi Siku ya Kiyama mtafufuliwa.
 
17Na kwa yakini tumeziumba juu yenu njia saba. Nasi hatukuwa wenye kughafilika na viumbe.
 
18Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi na tukayatuliza katika ardhi. Na hakika Sisi tunaweza kuyaondoa.
 
19Kwa maji hayo tukakufanyieni bustani za mitende na mizabibu, mnapata humo matunda mengi, na katika hayo mnakula;
 
20Na mti utokao katika mlima wa Sinai, unatoa mafuta na kuwa kitoweo kwa walao.
 
21Na hakika mnayo mazingatio makubwa katika nyama hoa - tunakunywesheni katika vile viliomo matumboni mwao, na nyinyi mnapata katika hao manufaa mengi, na pia mnawala.
 
22Na juu yao na juu ya marikebu mnabebwa.
 
23Na hakika tulimtuma Nuhu kwa watu wake, akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna mungu asiye kuwa Yeye. Basi je! Hamwogopi?
 
24Walisema wale wakuu walio kufuru katika watu wake: Huyu si chochote ila ni mtu tu kama nyinyi. Anataka kujipa ubora juu yenu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu amependa basi yakini angeli teremsha Malaika. Hatukusikia haya kwa baba zetu wa zamani.
 
25Huyu si lolote ila ni mtu mwenye wazimu. Basi mngojeeni tu kwa muda.
 
26Akasema (Nuhu): Mola wangu Mlezi! Ninusuru kwa kuwa wamenikanusha.
 
27Tukampa wahyi: Unda jahazi mbele ya macho yetu na uwongozi wetu! Basi itapo fika amri yetu na ikafurika tanuri, hapo waingize ndani yake wa kila namna dume na jike, na ahali zako, isipo kuwa yule ambaye katika wao juu yake imekwisha tangulia kauli. Wala usinitajie hao walio dhulumu. Kwani hao bila ya shaka watazamishwa.
 
28Basi utakapo tulia wewe na walio pamoja nawe humo marikebuni, sema: Alhamdulillahi Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, aliye tuokoa na watu madhaalimu!
 
29Na sema: Mola wangu Mlezi! Niteremshe mteremsho wenye baraka, na Wewe ni Mbora wa wateremshaji.
 
30Hakika katika hayo yapo mazingatio. Na kwa yakini Sisi ni wenye kuwafanyia mtihani.
 
31Kisha baada yao tukaanzisha kizazi kingine.
 
32Tukawapelekea Mtume miongoni mwao, kuwaambia: Muabuduni Mwenyezi Mungu! Hamna mungu asiye kuwa Yeye. Jee, hamwogopi?
 
33Na wakubwa katika watu wake walio kufuru na wakakanusha mkutano wa Akhera, na tukawadekeza kwa starehe katika maisha ya dunia, walisema: Huyu si chochote ila ni binaadamu kama nyinyi; anakula mlacho, na anakunywa mnywacho.
 
34Na nyinyi mkimt'ii mtu kama nyinyi basi hakika mtakuwa khasarani.
 
35Hivyo anakuahidini ati ya kwamba mtakapo kufa na mkawa udongo na mifupa kuwa mtatolewa?
 
36Hayawi! Hayawi hayo mnayo ahidiwa.
 
37Hapana ila uhai wetu wa duniani tu, tunakufa na kuishi basi. Wala sisi hatutafufuliwa.
 
38Huyu si lolote ila ni mtu anaye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo, wala sisi sio wa kumuamini.
 
39Akasema: Mola wangu Mlezi! Ninusuru kwa sababu wananikanusha.
 
40(Mwenyezi Mungu) akasema: Baada ya muda mchache watakuwa wenye kujuta.
 
41Basi ukawanyakua ukelele kwa haki, na tukawafanya kama takataka zinazo elea juu ya maji. Ikapotelea mbali kaumu ya madhaalimu!
 
42Kisha tukaleta baada yao vizazi vingine.
 
43Hapana umma uwezao kutanguliza ajali yake wala kuikawiza.
 
44Kisha tukawatuma Mitume wetu, mmoja baada ya mmoja. Kila umma alipo wafikia Mtume wao walimkanusha. Tukawafuatanisha hawa baada ya hawa, na tukawafanya ni hadithi za kusimuliwa. Wakapotelea mbali watu wasio amini.
 
45Kisha tukamtuma Musa na nduguye, Haaruni, pamoja na ishara zetu na hoja zilizo wazi.
 
46Kumwendea Firauni na wakuu wake. Lakini walijivuna, nao walikuwa watu majeuri.
 
47Wakasema: Je, tuwaamini wanaadamu wawili hawa kama sisi, na ambao watu wao ni watumwa wetu?
 
48Basi wakawakanusha, na wakawa miongoni mwa walio angamizwa.
 
49Na hakika tulimpa Musa Kitabu ili wapate kuongoka.
 
50Na tukamfanya mwana wa Mariamu na mama yake kuwa ni Ishara, na tukawapa makimbilio kwenda mahali palipo inuka penye utulivu na chemchem za maji.
 
51Enyi Mitume! Kuleni vyakula vizuri na tendeni mema. Hakika Mimi ni Mjuzi wa mnayo yatenda.
 
52Na kwa yakini huu Umma wenu ni Umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi, basi nicheni Mimi.
 
53Lakini walikatiana jambo lao mapande mbali mbali. Kila kundi likifurahia kwa waliyo nayo.
 
54Basi waache katika ghafla yao kwa muda.
 
55Je! Wanadhani ya kuwa kwa vile tunavyo wapa mali na watoto
 
56Ndio tunawahimizia kheri? Lakini wenyewe hawatambui.
 
57Kwa hakika hao ambao kwa kumwogopa Mola wao Mlezi wananyenyekea,
 
58Na wale ambao Ishara za Mola wao Mlezi wanaziamini,
 
59Na wale ambao Mola wao Mlezi hawamshirikishi,
 
60Na wale ambao wanatoa walicho pewa, na hali nyoyo zao zinagopa kwa kuwa watarejea kwa Mola wao Mlezi,
 
61Basi wote hao ndio wanao kimbilia katika mambo ya kheri, na ndio watakao tangulia kuyafikia.
 
62Na hatuilazimishi nafsi ila kwa kadri ya uwezo wake. Na tunacho kitabu kisemacho kweli. Nao hawatadhulumiwa.
 
63Lakini nyoyo zao zimeghafilika na hayo, na wanavyo vitendo vinginevyo wanavyo vifanya.
 
64Hata tutakapo watia katika adhabu wale walio dekezwa kwa starehe kati yao, hapo ndipo watapo yayatika.
 
65Msiyayatike leo! Hakika nyinyi hamtanusurika nasi.
 
66Hakika zilikuwa Aya zangu mkisomewa, nanyi mkirudi nyuma juu ya visigino vyenu,
 
67Na huku mkitakabari na usiku mkiizungumza (Qur'ani) kwa dharau.
 
68Je, hawakuifikiri kauli, au yamewajia yasiyo wafikia baba zao wa zamani?
 
69Au hawakumjua Mtume wao, ndio maana wanamkataa?
 
70Au wanasema: Ana wazimu? Bali amewajia kwa Haki, na wengi wao wanaichukia Haki.
 
71Na lau kuwa Haki ingeli fuata matamanio yao, basi zingeli haribika mbingu na ardhi na waliomo ndani. Bali tumewaletea ukumbusho wao, nao wanajitenga mbali na ukumbusho wao.
 
72Au unawaomba ujira? Lakini ujira wa Mola wako Mlezi ni bora, na Yeye ndiye Mbora wa wanao ruzuku.
 
73Na kwa yakini wewe unawaita kwenye Njia Iliyo Nyooka.
 
74Na hakika wale wasio iamini Akhera wanajitenga na Njia hiyo.
 
75Na lau tungeli warehemu na tukawaondolea shida waliyo nayo bila ya shaka wangeli endelea katika upotofu wao vile vile, wakitangatanga.
 
76Na hakika tuliwatia adhabu kali; lakini hawakuelekea kwa Mola wao Mlezi wala hawakunyenyekea.
 
77Mpaka tulipo wafungulia mlango wa adhabu kali, hapo ndipo wakawa wenye kukata tamaa.
 
78Na Yeye ndiye aliye kuumbieni kusikia na kuona na nyoyo za kufahamu. Ni kuchache mno kushukuru kwenu.
 
79Na Yeye ndiye aliye kuenezeni katika ardhi, na kwake Yeye mtakusanywa.
 
80Na Yeye ndiye anaye huisha na kufisha, na yake Yeye mabadiliko ya usiku na mchana. Basi je! Hamfahamu?
 
81Bali wanasema kama walivyo sema watu wa kwanza.
 
82Walisema: Je! Tukisha kufa tukawa udongo na mifupa ndio tutafufuliwa?
 
83Tuliahidiwa haya sisi na baba zetu zamani. Hayakuwa haya ila ni visa vya uwongo vya watu wa zamani.
 
84Sema: Ni ya nani ardhi na viliomo ndani yake, kama nyinyi mnajua?
 
85Watasema: Ni vya Mwenyezi Mungu! Sema: Basi, je, hamkumbuki?
 
86Sema: Ni nani Mola Mlezi wa mbingu saba na Mola Mlezi wa A'rshi Kuu?
 
87Watasema: Ni vya Mwenyezi Mungu. Sema: Basi je, hamwogopi?
 
88Sema: Ni nani mkononi mwake umo Ufalme wa kila kitu, naye ndiye anaye linda, wala hakilindwi asicho taka, kama mnajua?
 
89Watasema: (Ufalme huo) ni wa Mwenyezi Mungu. Sema: Basi vipi mnadanganyika?
 
90Bali tumewaletea Haki, na kwa yakini hao ni waongo.
 
91Mwenyezi Mungu hana mwana yeyote, wala hanaye mungu mwengine. Inge kuwa hivyo basi kila mungu angeli chukua alivyo umba, na baadhi yao wangeli washinda wengine. Mwenyezi Mungu ameepukana na sifa wanazo msifu.
 
92Mjuzi wa siri na dhaahiri, na ametukuka juu ya hayo wanayo mshirikisha nayo.
 
93Sema: Mola wangu Mlezi! Ukinionyesha adhabu waliyo ahidiwa,
 
94Mola wangu Mlezi! Usinijaalie katika watu madhaalimu hao.
 
95Na hakika Sisi ni waweza wa kukuonyeshsa tuliyo waahidi.
 
96Kinga maovu kwa kutenda yaliyo mema zaidi. Sisi tunajua wayasemayo.
 
97Na sema: Mola wangu Mlezi! Najikinga kwako na wasiwasi wa mashet'ani.
 
98Na najikinga kwako, Mola wangu Mlezi, wasinikaribie.
 
99Mpaka yanapo mfikia mmoja wao mauti, husema: Mola wangu Mlezi! Nirudishe.
 
100Ili nitende mema sasa badala ya yale niliyo yaacha. Wapi! Hii ni kauli aisemayo yeye tu. Na nyuma yao kipo kizuizi mpaka siku watapo fufuliwa.
 
101Basi litapo pulizwa baragumu hapo hautakuwapo ujamaa baina yao siku hiyo, wala hawataulizana.
 
102Ama wale ambao mizani zao zitakuwa nzito, hao ndio wenye kufanikiwa.
 
103Na wale ambao mizani zao zitakuwa nyepesi, hao ndio walio zitia khasarani nafsi zao, na katika Jahannamu watadumu.
 
104Moto utababua nyuso zao, nao watakuwa na nyuso zilizo kunjana.
 
105Je! Hazikuwa Aya zangu mkisomewa, na nyinyi mkizikanusha?
 
106Mola wetu Mlezi! Tulizidiwa na uovu wetu na tukawa watu tulio potea.
 
107Mola wetu Mlezi! Tutoe humu Motoni. Na tufanyapo tena basi kweli sisi ni wenye kudhulumu.
 
108Atasema Mwenyezi Mungu: Tokomeeni humo, wala msinisemeze.
 
109Bila ya shaka lilikuwapo kundi katika waja wangu likisema: Mola wetu Mlezi! Tumeamini; basi tusamehe na uturehemu, nawe ndiwe Mbora wa wanao rehemu.
 
110Lakini nyinyi mliwakejeli hata wakakusahaulisheni kunikumbuka, na mlikuwa mkiwacheka.
 
111Hakika Mimi leo nimewalipa kwa vile walivyo subiri. Bila ya shaka hao ndio wenye kufuzu.
 
112Atasema: Mlikaa muda gani katika ardhi kwa hisabu ya miaka?
 
113Watasema: Tulikaa siku moja au sehemu ya siku. Basi waulize wanao weka hisabu.
 
114Atasema: Nyinyi hamkukaa huko duniani ila kidogo, laiti ingeli kuwa mnajua.
 
115Je! Mlidhani ya kwamba tulikuumbeni bure na ya kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa?
 
116Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa Haki, hapana mungu ila Yeye, Mola Mlezi wa A'rshi Tukufu.
 
117Na anaye muomba - pamoja na Mwenyezi Mungu - mungu mwenginewe hana ushahidi wa hili; basi bila ya shaka hisabu yake iko kwa Mola wake Mlezi. Kwa hakika makafiri hawafanikiwi.
 
118Nawe sema: Mola wangu Mlezi! Samehe na urehemu nawe ni Mbora wa wanao rehemu.
 
 
ReadTheQuran.org