Translations Suras
KISWAHILI

20 - T'AHA

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

 
1T'AHA!
 
2Hatukukuteremshia Qur'ani ili upate mashaka.
 
3Bali ni mawaidha kwa wenye kunyenyekea.
 
4Materemsho yatokayo kwa aliye umba ardhi na mbingu zilizo juu.
 
5Arrahmani, Mwingi wa Rehema, aliye tawala juu ya Kiti cha Enzi.
 
6Ni vyake vyote viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi, na viliomo baina yao, na viliomo chini ya ardhi.
 
7Na ukinyanyua sauti kwa kusema...basi hakika Yeye anajua siri na duni kuliko siri.
 
8Mwenyezi Mungu! Hapana mungu isipo kuwa Yeye. Yeye ana majina mazuri kabisa.
 
9Na je! Imekufikia hadithi ya Musa?
 
10Alipo uona moto, akawaambia watu wake: Ngojeni! Mimi nimeuona moto, huenda nikakuleteeni kijinga kutoka huo moto, au nikapata uongofu kwenye moto.
 
11Basi alipo ufikia akaitwa: Ewe Musa!
 
12Hakika Mimi ndiye Mola wako Mlezi! Basi vua viatu vyako. Kwani upo katika bonde takatifu la T'uwa.
 
13Nami nimekuteua wewe; basi sikiliza unayo funuliwa.
 
14Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu. Hapana mungu ila Mimi tu. Basi niabudu Mimi, na ushike Sala kwa ajili ya kunikumbuka Mimi.
 
15Hakika Saa itakuja bila ya shaka. Nimekaribia kuificha, ili kila nafsi ilipwe kwa iliyo yafanya.
 
16Kwa hivyo asikukengeushe nayo yule ambaye haiamini na akafuata pumbao lake ukaja kuhiliki.
 
17Na nini hicho kilichomo mkononi mwako wa kulia, ewe Musa?
 
18Akasema: Hii ni fimbo yangu; naiegemea na ninawaangushia majani kondoo na mbuzi wangu. Tena inanifaa kwa matumizi mengine.
 
19Akasema: Itupe, ewe Musa!
 
20Akaitupa. Mara ikawa nyoka anaye kwenda mbio.
 
21Akasema: Ikamate, wala usiogope! Tutairudisha hali yake ya kwanza.
 
22Na uambatishe mkono wako kwenye ubavu. Utatoka mweupe pasipo kuwa na madhara yoyote. Hiyo ni ishara nyengine.
 
23Ili tukuonyeshe baadhi ya ishara zetu kubwa.
 
24Nenda kwa Firauni; kwani hakika yeye amepindukia mipaka.
 
25(Musa) akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Nikunjulie kifua changu,
 
26Na unifanyie nyepesi kazi yangu,
 
27Na ulifungue fundo lililo katika ulimi wangu,
 
28Wapate kufahamu maneno yangu.
 
29Na nipe waziri katika watu wangu,
 
30Harun, ndugu yangu.
 
31Kwake yeye niongeze nguvu zangu.
 
32Na umshirikishe katika kazi yangu.
 
33Ili tukutakase sana.
 
34Na tukukumbuke sana.
 
35Hakika Wewe unatuona.
 
36Akasema: Hakika Umepewa maombi yako, ewe Musa!
 
37Na hakika tulikwisha kufanyia hisani mara nyengine...
 
38Pale tulipo mfunulia mama yako yaliyo funuliwa,
 
39Ya kuwa mtie katika kisanduku, na kisha kitie mtoni, na mto utamfikisha ufukweni. Atamchukua adui yangu naye ni adui yake. Na nimekutilia mapenzi yanayo tokana kwangu, na ili ulelewe machoni mwangu.
 
40Dada yako alipo kwenda na akasema: Je! Nikujuulisheni mtu wa kuweza kumlea? Basi tukakurejesha kwa mama yako ili macho yake yaburudike, wala asihuzunike. Na ulimuuwa mtu, nasi tukakuokoa katika dhiki, na tukakujaribu kwa majaribio mengi. Ukakaa miaka kwa watu wa Madyana. Kisha ukaja kama ilivyo kadiriwa, ewe Musa!
 
41Na nimekuteuwa kwa ajili ya nafsi yangu.
 
42Nenda, wewe na ndugu yako, pamoja na ishara zangu, wala msichoke kunikumbuka.
 
43Nendeni kwa Firauni. Hakika yeye amepindukia mipaka.
 
44Mwambieni maneno laini, huenda akazingatia au akaogopa.
 
45Wakasema: Ewe Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tunaogopa asije akapindukia mipaka juu yetu au kufanya jeuri.
 
46Akasema: Msiogope! Hakika Mimi ni pamoja nanyi. Nasikia na ninaona.
 
47Basi mwendeeni, na mwambieni: Hakika sisi ni Mitume wa Mola wako Mlezi! Basi waache Wana wa Israili watoke nasi, wala usiwaadhibu. Sisi tumekuletea ishara itokayo kwa Mola wako Mlezi. Na amani itakuwa juu ya aliye fuata uwongofu.
 
48Hakika tumefunuliwa sisi kwamba hapana shaka adhabu itamsibu anaye kadhibisha na akapuuza.
 
49(Firauni) akasema: Basi Mola wenu Mlezi ni nani, ewe Musa?
 
50Akasema: Mola wetu Mlezi ni yule aliye kipa kila kitu umbo lake, kisha akakiongoa.
 
51Akasema: Nini hali ya karne za kwanza?
 
52Akasema: Ilimu yake iko kwa Mola wangu Mlezi katika Kitabu. Mola wangu Mlezi hapotei wala hasahau.
 
53Ambaye amekufanyieni ardhi kuwa tandiko, na akakupitishieni humo njia, na akakuteremshieni kutoka mbinguni maji. Na kwa hayo tukatoa namna mbali mbali za mimema.
 
54Kuleni, na mchunge wanyama wenu. Hakika katika hayo zipo ishara kwa wenye akili.
 
55Kutokana nayo (ardhi) tumekuumbeni, na humo tunakurudisheni, na kutoka humo tutakutoeni mara nyengine.
 
56Na hakika tulimwonyesha ishara zetu zote. Lakini alikadhibisha na akakataa.
 
57Akasema: Ewe Musa! Hivyo umetujia kututoa katika nchi yetu kwa uchawi wako?
 
58Basi sisi hakika tutakueletea uchawi kama huo. Basi weka miadi baina yetu na wewe, ambayo tusiivunje sisi wala wewe, mahali patapo kuwa sawa.
 
59Akasema: Miadi yenu ni siku ya Sikukuu; na watu wakusanywe kabla ya adhuhuri.
 
60Basi Firauni akarudi na akatengeneza hila yake, kisha akaja.
 
61Musa akamwambia: Ole wenu! Msimzulie Mwenyezi Mungu uwongo, asije akakufutilieni mbali kwa adhabu. Na mwenye kuzua lazima ashindwe!
 
62Basi wakazozana kwa shauri yao wenyewe kwa wenyewe, na wakanong'ona kwa siri.
 
63Wakasema: Hakika hawa wawili ni wachawi, wanataka kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wao, na waondoe mila zenu zilizo bora kabisa.
 
64Kwa hivyo kusanyeni hila zenu zote, kisha mfike kwa kujipanga safu, na kwa yakini atafuzu kweli kweli leo atakaye shinda.
 
65Wakasema: Ewe Musa! Je! Utatupa wewe, au tutakuwa sisi wa kwanza kutupa?
 
66Akasema: Bali tupeni nyinyi! Tahamaki kamba zao na fimbo zao zikaonekana mbele yake, kwa uchawi wao, kuwa zinapiga mbio.
 
67Basi Musa akaingia khofu nafsi yake.
 
68Tukasema: Usikhofu! Hakika wewe ndiye utakaye shinda.
 
69Na kitupe kilicho katika mkono wako wa kulia; kitavimeza walivyo viunda. Hakika walivyo unda ni hila za mchawi tu, na mchawi hafanikiwi popote afikapo.
 
70Basi wachawi wakaangushwa wanasujudu. Wakasema: Tumemuamini Mola Mlezi wa Harun na Musa!
 
71(Firauni) akasema: Oh! Mnamuamini kabla sijakupeni ruhusa? Hakika yeye ndiye mkubwa wenu aliye kufundisheni uchawi. Basi kwa yakini nitakukateni mikono yenu na miguu yenu kwa kutafautisha. Na nitakutundikeni misalabani katika vigogo vya mitende, na hapo kwa yakini mtajua ni nani katika sisi aliye mkali wa kuadhibu na kuiendeleza adhabu yake.
 
72Wakasema: Hatutokukhiari wewe kuliko ishara waziwazi zilizo tujia, na kuliko yule aliye tuumba. Basi hukumu utavyo hukumu; kwani wewe unahukumu haya ya maisha ya duniani tu.
 
73Hakika sisi tumemuamini Mola wetu Mlezi ili atusamehe makosa yetu na uchawi ulio tulazimisha kuufanya. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mbora na Mwenye kudumu zaidi.
 
74Hakika ataye mjia Mola wake Mlezi naye ni mkhalifu, basi kwa yakini, yake huyo ni Jahannamu. Hafi humo wala haishi.
 
75Na atakaye mjia naye ni Muumini aliye tenda mema, basi hao ndio wenye vyeo vya juu.
 
76Bustani za milele zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Na hayo ni malipo ya mwenye kujitakasa.
 
77Na tulimfunulia Musa: Toka usiku na waja wangu, na uwapigie njia kavu baharini. Usikhofu kukamatwa, wala usiogope.
 
78Firauni akawafuata pamoja na majeshi yake. Basi kiliwafudikiza humo baharini kilicho wafudikiza.
 
79Na Firauni aliwapoteza watu wake wala hakuwaongoa.
 
80Enyi Wana wa Israili! Hakika tulikuokoeni na adui yenu, na tukakuahidini upande wa kulia wa mlima. Na tulikuteremshieni Manna na Salwa.
 
81Kuleni katika vitu vizuri hivyo tulivyo kuruzukuni, wala msiruke mipaka katika hayo, isije ikakushukieni ghadhabu yangu. Na inaye mshukia ghadhabu yangu basi huyo ameangamia.
 
82Na hakika Mimi ni Mwingi wa Kusamehe kwa anaye tubia, na akaamini, na akatenda mema, tena akaongoka.
 
83Na nini kilicho kutia haraka ukawaacha watu wako, ewe Musa?
 
84Akasema: Hao wapo nyuma yangu wananifuatia. Na nimefanya haraka kukujia, Mola wangu Mlezi, ili uridhike.
 
85(Mwenyezi Mungu) akasema: Sisi tumewatia mtihani watu wako baada yako, na Msamaria amewapoteza.
 
86Musa akarudi kwa watu wake kwa ghadhabu na kusikitika. Akasema: Enyi watu wangu! Kwani Mola wenu Mlezi hakukuahidini ahadi nzuri? Je, umekuwa muda mrefu kwenu au mmetaka ikushukieni ghadhabu ya Mola wenu Mlezi, ndio maana mkavunja miadi yangu?
 
87Wakasema: Sisi hatukuvunja miadi yako kwa khiari yetu, lakini tulibebeshwa mizigo ya mapambo ya watu, basi tukaitupa. Na hivyo ndivyo alivyo toa shauri Msamaria.
 
88Na akawaundia ndama, kiwiliwili chenye sauti. Na wakasema: Huyu ndiye mungu wenu, na mungu wa Musa, lakini alisahau.
 
89Je! Hawakuona kuwa hakuwarudishia neno, wala hakuweza kuwadhuru wala kuwafaa?
 
90Na hakika Harun alikwisha waambia kabla yake: Enyi watu wangu! Hakika nyinyi mmetiwa mtihanini tu kwa kitu hiki. Na kwa yakini Mola wenu Mlezi ni Arrahmani, Mwingi wa Rehema. Basi nifuateni mimi, na t'iini amri yangu!
 
91Wakasema: Hatutaacha kumuabudu mpaka Musa atapo rejea kwetu.
 
92(Musa) akasema: Ewe Harun! Ni nini kilicho kuzuia, ulipo waona wamepotea,
 
93Hata usinifuate? Je, umeasi amri yangu?
 
94Akasema: Ewe mwana wa mama yangu! Usinishike ndevu zangu, wala kichwa changu. Kwa hakika naliogopa usije sema: Umewafarikisha Wana wa Israil, na hukungojea kauli yangu.
 
95(Musa) akasema: Ewe Msamaria! Unataka nini ?
 
96Akasema: Niliona wasiyo yaona wao, nikashika gao katika unyao wa Mtume. Kisha nikalitupa. Na hivi ndivyo ilivyo nielekeza nafsi yangu.
 
97(Musa) akasema: Basi ondoka! Na kwa yakini utakuwa katika maisha ukisema: Usiniguse. Na hakika una ahadi kwako isiyo vunjwa. Na mtazame huyo mungu wako uliye endelea kumuabudu - Sisi kwa hakika tutamchoma moto, kisha tutamtawanya baharini atawanyike.
 
98Hakika Mungu wenu ni Allah, Mwenyezi Mungu, tu. Hapana Mungu isipo kuwa Yeye. Ujuzi wake umeenea kila kitu.
 
99Namna hivi tunakuhadithia katika khabari za yaliyo tangulia. Na hakika tumekuletea kutoka kwetu mawaidha ya kukumbukwa.
 
100Atakaye jitenga nayo, basi kwa yakini Siku ya Kiyama atabeba mzigo.
 
101Wadumu humo. Na ni mzigo muovu kwao kuubeba Siku ya Kiyama!
 
102Siku litakapo pulizwa barugumu, na tukawakusanya wakhalifu Siku hiyo, hali macho yao ya kibuluu.
 
103Watanong'onezana wao kwa wao: Hamkukaa ila siku kumi tu.
 
104Sisi tunajua zaidi watakayo yasema, atakapo sema mbora wao katika mwendo: Nyinyi hamkukaa ila siku moja tu.
 
105Na wanakuuliza khabari za milima. Waambie: Mola wangu Mlezi ataivuruga vuruga.
 
106Na ataiacha tambarare, uwanda.
 
107Hutaona humo mdidimio wala muinuko.
 
108Siku hiyo watamfuata muitaji asiye na upotofu. Na sauti zote zitamnyenyekea Arrahmani Mwingi wa Rahema. Basi husikii ila mchakato na mnong'ono.
 
109Siku hiyo uombezi haufai kitu, ila wa aliye mruhusu Arrahmani Mwingi wa Rehema na akamridhia kusema.
 
110Yeye anajua yaliyo mbele yao, na yaliyo nyuma yao. Wala wao hawawezi kumjua Yeye vilivyo.
 
111Na zitadhalilika nyuso mbele ya Aliye Hai Milele, Mwangalizi Mkuu. Na atakuwa ameharibikiwa mwenye kubeba dhulma.
 
112Na anaye tenda mema, naye ni Muumini, basi hatakhofu kudhulumiwa wala kupunjwa.
 
113Na namna hivi tumeiteremsha Qur'ani kwa Kiarabu, na tumekariri humo maonyo ili wapate kuogopa na kujilinda na iwaletee makumbusho.
 
114Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa Haki. Wala usiifanyie haraka hii Qur'ani, kabla haujamalizika ufunuo wake. Na sema: Mola wangu Mlezi! Nizidishie ilimu.
 
115Na hapo zamani tuliagana na Adam, lakini alisahau, wala hatukuona kwake azma kubwa.
 
116Na tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam! Wakasujudu, isipo kuwa Iblisi, alikataa.
 
117Tukasema: Ewe Adam! Hakika huyu ni adui yako na wa mkeo. Basi asikutoeni katika Bustani hii, mkaingia mashakani.
 
118Hakika humo hutakuwa na njaa wala hutakuwa uchi.
 
119Na hakika hutapata kiu humo wala hutapata joto.
 
120Lakini Shet'ani alimtia wasiwasi, akamwambia: Ewe Adam! Nikujuulishe mti wa kuishi milele na ufalme usio koma?
 
121Basi wakaula wote wawili, na uchi wao ukawadhihirikia na wakaanza kujibandika majani ya Bustani. Na Adam akamuasi Mola wake Mlezi, na akapotea njia.
 
122Kisha Mola wake Mlezi akamteuwa, naye akamkubalia toba yake, naye akamwongoa.
 
123Akasema: Ondokeni humu nyote, hali ya kuwa ni maadui nyinyi kwa nyinyi. Na ukikufikieni uwongofu kutoka kwangu basi atakaye ufuata uwongofu wangu, hatapotea wala hatataabika.
 
124Na atakaye jiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu.
 
125Aseme: Ewe Mola wangu Mlezi! Mbona umenifufua kipofu, nami nilikuwa nikiona?
 
126(Mwenyezi Mungu) atasema: Ndivyo vivyo hivyo. Zilikufikia ishara zetu, nawe ukazisahau; na kadhaalika leo unasahauliwa.
 
127Na hivi ndivyo tutakavyo mlipa kila apitaye kiasi, na asiye amini ishara za Mola wake Mlezi. Na hakika adhabu ya Akhera ni kali zaidi, na inadumu zaidi.
 
128Je! Haikuwabainikia tu; vizazi vingapi tuliviangamiza kabla yao, nao wanatembea katika maskani zao? Hakika katika hayo zimo ishara kwa wenye akili.
 
129Na lau kuwa si neno lililo kwisha tangulia kutoka kwa Mola wako Mlezi na muda ulio wekwa, bila ya shaka inge fika adhabu (hapa hapa).
 
130Yavumilie haya wayasemayo. Na umtakase Mola wako Mlezi kwa kumsifu kabla ya kuchomoza jua, na kabla halijachwa, na nyakati za usiku pia umtakase, na ncha za mchana ili upate ya kukuridhisha.
 
131Wala usivikodolee macho tulivyo wastareheshea baadhi ya watu miongoni mwao, kwa ajili ya mapambo ya duniani, ili tuwajaribu. Na riziki ya Mola wako Mlezi ni bora na inadumu zaidi.
 
132Na waamrishe watu wako kusali, na uendelee mwenyewe kwa hayo. Sisi hatukuombi wewe riziki, bali Sisi ndio tunakuruzuku. Na mwisho mwema ni kwa mchamngu.
 
133Na walisema: Kwa nini hakutuletea muujiza kutoka kwa Mola wake Mlezi? Je! Haikuwafikilia dalili wazi ya yaliyomo katika Vitabu vya kale?
 
134Na lau kuwa tuliwaangamiza kwa adhabu kabla yake, wangeli sema: Ewe Mola wetu Mlezi! Kwa nini usituletee Mtume tukazifuata ishara zako kabla hatujadhilika na kuhizika.
 
135Sema: Kila mmoja anangoja. Basi ngojeni! Hivi karibuni mtajua nani mwenye njia sawa na nani aliye ongoka.
 
 
ReadTheQuran.org