Translations Suras
KISWAHILI

16 - AN NAH'L

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

 
1Amri ya Mwenyezi Mungu itafika tu. Basi msiihimize. Ametakasika na Ametukuka na wanayo mshirikisha nayo.
 
2Huwateremsha Malaika na Roho kwa amri yake juu ya amtakaye katika waja wake ili nyinyi muonye kwamba hapana mungu ila Mimi, basi nicheni Mimi.
 
3Ameziumba mbingu na ardhi kwa Haki. Ametukuka na wanayo shirikisha.
 
4Amemuumba mtu kwa tone la manii. Naye mara amekuwa mshindani dhaahiri.
 
5Na nyama hoa amekuumbieni. Katika hao mna vifaa vya kutia joto, na manufaa mengineyo, na baadhi yao mnawala.
 
6Na wanakupeni furaha pale mnapo warudisha jioni na mnapo wapeleka malishoni asubuhi.
 
7Na hubeba mizigo yenu kupeleka kwenye miji msiyo weza kuifikia ila kwa mashaka ya nafsi. Hakika Mola wenu Mlezi ni Mpole na Mwenye kurehemu.
 
8Na farasi, na nyumbu, na punda ili muwapande, na kuwa ni pambo. Na ataumba msivyo vijua.
 
9Na ni juu ya Mwenyezi Mungu kuelekeza Njia. Na zipo njia za upotovu. Na angeli penda angeli kuongoeni nyote.
 
10Yeye ndiye anaye kuteremshieni maji kutoka mbinguni. Katika hayo nyinyi mnapata ya kunywa, na miti ya kulishia.
 
11Kwa hayo Yeye anaizalisha kwa ajili yenu mimea, na mizaituni, na mitende, na mizabibu, na kila namna ya matunda. Hakika katika haya zipo ishara kwa watu wanao fikiri.
 
12Na amefanya ukutumikieni usiku na mchana, na jua na mwezi, na nyota zikutumikieni kwa amri yake. Hakika katika hayo zipo ishara kwa watu wenye akili.
 
13Na hivi alivyo vieneza katika ardhi vya rangi mbali mbali. Hakika katika hayo ipo ishara kwa watu wanao waidhika.
 
14Yeye ndiye aliye ifanya bahari ikutumikieni, ili kutokana na humo mpate kula nyama laini, na mtoe humo mapambo mnayo yavaa. Na unaona marikebu zikikata maji humo, ili mtafute fadhila yake, na mpate kushukuru.
 
15Na kaweka katika ardhi milima ili ardhi isiyumbe yumbe nanyi. Na mito, na njia ili mpate kuongoka.
 
16Na alama nyengine. Na kwa nyota wao wanajiongoza.
 
17Ati anaye umba ni kama asiye umba? Basi hebu, hamkumbuki?
 
18Na mkizihisabu neema za Mwenyezi Mungu, hamwezi kuzidhibiti. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira, Mwenye kurehemu.
 
19Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yaficha na mnayo yatangaza.
 
20Na wale wanao waomba wasio kuwa Mwenyezi Mungu hawaumbi kitu, bali wao wameumbwa.
 
21Ni wafu si wahai, na wala hawajui watafufuliwa lini.
 
22Mungu wenu ni Mungu Mmoja. Lakini wasio iamini Akhera nyoyo zao zinakataa, nao wanajivuna.
 
23Hapana shaka kuwa hakika Mwenyezi Mungu anayajua wanayo yaficha na wanayo yatangaza. Kwa hakika Yeye hawapendi wanao jivuna.
 
24Na wanapo ambiwa: Kateremsha nini Mola wenu Mlezi? Husema: Hadithi za kubuni za watu wa kale!
 
25Ili wabebe mizigo yao kwa ukamilifu Siku ya Kiyama, na sehemu ya mizigo ya wale wanao wapoteza bila ya kujua. Angalia, ni maovu mno hayo wanayo yabeba!
 
26Walipanga vitimbi walio kuwa kabla yao, Mwenyezi Mungu akayasukua majengo yao kwenye misingi, dari zikawaporomokea juu yao, na adhabu ikawajia kutoka wasipo kujua.
 
27Kisha Siku ya Kiyama atawahizi na atasema: Wako wapi hao washirika wangu ambao kwao mkiwakutisha (Manabii) mashaka? Watasema walio pewa ilimu: Hakika leo ndiyo hizaya na adhabu itawashukia makafiri,
 
28Ambao Malaika waliwafisha nao wamejidhulumu nafsi zao! Basi watasalimu amri, waseme: Hatukuwa tukifanya uovu wowote. (Wataambiwa): Kwani! Hakika Mwenyezi Mungu anajua sana mliyo kuwa mkiyatenda.
 
29Basi ingieni milango ya Jahannamu, humo mdumu. Ni maovu mno makaazi ya wafanyao kiburi!
 
30Na wataambiwa walio mcha Mungu: Mola wenu Mlezi kateremsha nini? Watasema: Kheri. Walio fanya wema katika dunia hii watapata wema. Na nyumba ya Akhera ni bora zaidi, na njema mno nyumba ya wachamngu.
 
31Bustani za milele wataziingia; iwe inapita kati yake mito. Humo watapata watakacho. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu awalipavyo wenye kumcha.
 
32Wale ambao Malaika huwafisha katika hali njema, wanawaambia: Amani iwe juu yenu! Ingieni Peponi kwa sababu ya yale mliyo kuwa mkiyatenda.
 
33Wanangojea jengine hawa ila Malaika wawafikie, au iwafikie amri ya Mola wako Mlezi? Kama hivyo walitenda walio kuwa kabla yao. Na Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu, lakini walijidhulumu wenyewe.
 
34Basi ukawafikia uovu wa waliyo yatenda, na waliyo kuwa wakiyakejeli yakawazunguka.
 
35Na washirikina wanasema: Mwenyezi Mungu angeli taka tusingeli abudu chochote badala yake, sisi wala baba zetu, wala tusingeli harimisha chochote bila ya Yeye. Kama hivyo walifanya walio kuwa kabla yao. Basi lipo lolote juu ya Mitume isipo kuwa kubalighisha kwa uwazi?
 
36Na kwa hakika kwa kila umma tuliutumia Mtume kwamba: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na muepukeni Shetani. Basi kati yao wapo alio waongoa Mwenyezi Mungu. Na kati yao wapo ambao ulio wathibitikia upotovu. Basi tembeeni katika ardhi, muangalie ulikuwaje mwisho wa wanao kanusha.
 
37Hata ukiwa na pupa ya kutaka kuwaongoa, lakini Mwenyezi Mungu hamwongoi yule anaye shikilia kupotea. Wala hawatapata wa kuwanusuru.
 
38Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu ukomo wa viapo vyao kwamba Mwenyezi Mungu hatomfufua aliye kufa. Kwani! Ni ahadi iliyo juu yake kikweli; lakini watu wengi hawajui.
 
39Ili kuwabainishia yale waliyo khitalifiana, na ili wajue walio kufuru kwamba wao walikuwa ni waongo.
 
40Kauli yetu kwa kitu tunacho kitaka kiwe, ni kukiambia: Kuwa! Basi kinakuwa.
 
41Na wale walio hama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu baada ya kudhulumiwa, bila ya shaka tutawaweka duniani kwa wema; na ujira wa Akhera ni mkubwa zaidi; laiti kuwa wanajua!
 
42Wale wanao subiri na wakamtegemea Mola wao Mlezi.
 
43Nasi hatukuwatuma kabla yako ila watu wanaume tulio wapa Wahyi (Ufunuo). Basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui
 
44Kwa Ishara wazi na Vitabu. Nasi tumekuteremshia wewe Ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyo teremshwa kwao, wapate kufikiri.
 
45Je! Wameaminisha wanao fanya vitimbi vya uovu kwamba Mwenyezi Mungu hatawadidimiza katika ardhi, na haitawafika adhabu kutoka wasipo pajua?
 
46Au hatawashika katika nyendo zao, na wala hawataponyoka?
 
47Au hatawashika kwa kitisho na kuwapunguza kidogo kidogo? Hakika Mola wenu Mlezi ni Mwenye huruma, Mwenye kurehemu.
 
48Je! Hawavioni vitu alivyo viumba Mwenyezi Mungu - vivuli vyao vinaelekea kushotoni na kuliani, kumsujudia Mwenyezi Mungu na vikinyenyekea?
 
49Na vyote viliomo katika mbingu na katika ardhi, tangu wanyama mpaka Malaika, vinamsujuidia Mwenyezi Mungu, na wala havitakabari.
 
50Vinamkhofu Mola wao Mlezi aliye juu yao, na vinafanya vinavyo amrishwa.
 
51Na Mwenyezi Mungu amesema: Msiwe na miungu wawili! Hakika Yeye ni Mungu Mmoja. Basi niogopeni Mimi tu!
 
52Na ni vyake Yeye viliomo katika mbingu na ardhi. Na Dini ni yake Yeye daima. Je! Mtamcha mwengine asiye kuwa Mwenyezi Mungu?
 
53Na neema yoyote mliyo nayo inatoka kwa Mwenyezi Mungu. Kisha yakikuguseni madhara mnamyayatikia Yeye.
 
54Na anapo kuondosheeni madhara mara kundi moja miongoni mwenu linamshirikisha Mola wao Mlezi,
 
55Wakizikataa neema tulizo wapa. Basi stareheni. Mtakuja jua!
 
56Na hao ambao hata hawawajui wanawawekea sehemu ya tunavyo waruzuku. Wallahi! Bila ya shaka mtasailiwa kwa hayo mliyo kuwa mnayazua!
 
57Na wanamfanyia Mwenyezi Mungu ati ana mabinti, Subhanahu, Aliye takasika! Na wao wenyewe, ati ndio wawe na hayo wanayo yatamani!
 
58Na mmoja wao akibashiriwa kwa msichana, uso wake unasawijika, naye kajaa chuki.
 
59Anajificha asionekane na watu kwa ubaya wa aliyo bashiriwa! Je, akae naye juu ya fedheha hiyo au amfukie udongoni? Tazama uovu wa wanavyo hukumu!
 
60Hali ya wasio iamini Akhera ni ovu; na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye sifa tukufu. Naye ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
 
61Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli wachukulia watu kwa mujibu wa dhulma zao, basi asingeli mwacha hapa hata mnyama mmoja. Lakini anawaakhirisha mpaka muda ulio wekwa. Na unapo fika muda wao hawatakawilia hata saa moja wala hawatatangulia.
 
62Na wanampa Mwenyezi Mungu wanavyo vichukia wao, na ndimi zao zinasema uwongo kwamba wao watapata mema. Hapana shaka hakika wamewekewa Moto, nao wataachwa humo.
 
63Wallahi! Sisi tulituma Mitume kwa umati zilizo kuwa kabla yako, lakini Shetani aliwapambia vitendo vyao. Kwa hivyo leo yeye ndiye rafiki yao; nao watapata adhabu chungu.
 
64Na hatukukuteremshia Kitabu isipo kuwa uwabainishie yale ambayo wanakhitalifiana, na kiwe Uwongofu na Rehema kwa watu wanao amini.
 
65Na Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni na kwa hayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Kwa hakika katika hayo imo Ishara kwa watu wanao sikia.
 
66Na hakika katika nyama hoa nyinyi mna mazingatio. Tunakunywesheni katika vile viliomo matumboni mwao, vikatoka baina ya mavi na damu, maziwa safi mazuri kwa wanywao.
 
67Na kutokana na matunda ya mitende na mizabibu mnatengeneza ulevi na riziki nzuri. Hakika katika hayo ipo Ishara kwa wanao tumia akili.
 
68Na Mola wako Mlezi amemfunulia nyuki: Jitengenezee majumba yako katika milima,na katika miti, na katika wanayo jenga watu.
 
69Kisha kula katika kila matunda, na upite katika njia za Mola wako Mlezi zilizo fanywa nyepesi kuzipita. Na kutoka matumbo yao kinatoka kinywaji chenye rangi mbali mbali; ndani yake kina matibabu kwa wanaadamu. Hakika katika haya ipo Ishara kwa watu wanao fikiri.
 
70Na Mwenyezi Mungu amekuumbeni; kisha anakufisheni. Na miongoni mwenu wapo wanao rudishwa kwenye umri mbaya kabisa, hata akawa asijue kitu baada ya ujuzi alio kuwa nao. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi na Mweza.
 
71Na Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine katika riziki. Na wale walio fadhilishwa hawarudishi riziki zao kwa wale ilio wamiliki mikono yao ya kulia ili wawe sawa katika riziki hiyo. Basi je, wanazikataa neema za Mwenyezi Mungu?
 
72Na Mwenyezi Mungu amekuumbieni wake katika jinsi yenu, na akakujaalieni kutoka kwa wake zenu wana na wajukuu, na akakuruzukuni vitu vizuri vizuri. Basi je, wanaamini upotovu na wanazikataa neema za Mwenyezi Mungu?
 
73Na badala ya Mwenyezi Mungu wanawaabudu wasio wamilikia riziki kutoka mbinguni wala kwenye ardhi, wala hawawezi kitu.
 
74Basi msimpigie Mwenyezi Mungu mifano. Hakika Mwenyezi Mungu anajua, na nyinyi hamjui.
 
75Mwenyezi Mungu anapiga mfano wa mtumwa aliye milikiwa, asiye weza kitu, na mwingine tuliye mruzuku riziki njema inayo toka kwetu, naye akawa anatoa katika riziki hiyo kwa siri na dhaahiri. Je, hao watakuwa sawa? Alhamdu Lillahi! Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui.
 
76Na Mwenyezi Mungu anapiga mfano wa watu wawili. Mmoja wao ni bubu, hawezi chochote, naye ni mzigo kwa bwana wake. Popote anapo muelekeza haleti kheri. Je! Huyo anaweza kuwa sawa na yule anaye amrisha uadilifu, naye yuko juu ya Njia Iliyo Nyooka?
 
77Na siri zote za katika mbingu na ardhi ziko kwa Mwenyezi Mungu. Wala halikuwa jambo la Saa (ya Kiyama) ila kama kupepesa kwa jicho, au akali ya hivyo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
 
78Na Mwenyezi Mungu amekutoeni matumboni mwa mama zenu, hali ya kuwa hamjui kitu, na amekujaalieni masikio na macho na nyoyo ili mpate kushukuru.
 
79Je! Hawawaoni ndege walivyo wat'iifu katika anga la mbingu? Hapana mwenye kuwashika isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Hakika katika haya zipo ishara kwa watu wanao amini.
 
80Na Mwenyezi Mungu amekujaalieni majumba yenu yawe ni maskani yenu, na amekujaalieni kutokana na ngozi za wanyama nyumba mnazo ziona nyepesi wakati wa safari zenu na wakati wa kutua kwenu. Na kutokana na sufi zao na manyoya yao na nywele zao mnafanya matandiko na mapambo ya kutumia kwa muda.
 
81Na Mwenyezi Mungu amekufanyieni vivuli katika vitu alivyo viumba, na amekufanyieni maskani milimani, na amekufanyieni nguo za kukingeni na joto, na nguo za kukingeni katika vita vyenu. Ndio hivyo anakutimizieni neema zake ili mpate kut'ii.
 
82Basi wakikengeuka lilio juu yako wewe ni kufikisha ujumbe wazi wazi.
 
83Wanazijua neema za Mwenyezi Mungu, kisha wanazikanusha; na wengi wao ni makafiri.
 
84Na siku tutakapo wainua kutokana na kila umma shahidi, kisha hawataruhusiwa walio kufuru wala hawataachiliwa kutaka radhi.
 
85Na walio dhulumu watakapo iona adhabu hawatapunguziwa hiyo adhabu, wala hawatapewa muhula.
 
86Na walio shirikisha watakapo waona hao walio washirikisha na Mwenyezi Mungu, watasema: Mola wetu Mlezi! Hawa ndio washirikishwa wetu ambao tulikuwa tukiwaabudu badala yako. Ndipo wale watakapo watupia kauli: Hakika nyinyi ni waongo!
 
87Na siku hiyo watasalimu amri mbele ya Mwenyezi Mungu, na yatapotea waliyo kuwa wakiyazua.
 
88Wale walio kufuru na kuzuilia Njia ya Mwenyezi Mungu tutawazidishia adhabu juu ya adhabu, kwa walivyo kuwa wakifisidi.
 
89Na (waonye) siku tutakapo wainua mashahidi katika kila umma wakiwashuhudia kwa yanayo tokana na wao, na tutakuleta wewe uwe shahidi juu ya hao. Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinacho bainisha kila kitu, na ni uwongofu, na rehema, na bishara kwa Waislamu.
 
90Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu, na hisani, na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, na uovu, na dhulma. Anakuwaidhini ili mpate kukumbuka.
 
91Na timizeni ahadi ya Mwenyezi Mungu mnapo ahidi, wala msivunje viapo baada ya kuvithibitisha, ilihali mmekwisha mfanya Mwenyezi Mungu ndiye mdhamini wenu. Hakika Mwenyezi Mungu anayajua myatendayo.
 
92Wala msiwe kama mwanamke anaye uzongoa uzi wake baada ya kwisha usokota ukawa mgumu. Mnavifanya viapo vyenu kuwa ni njia ya kudanganyana baina yenu kwa kuwa ati taifa moja lina nguvu zaidi kuliko jengine? Hakika Mwenyezi Mungu anakujaribuni kwa njia hiyo. Na bila ya shaka atakubainishieni Siku ya Kiyama mliyo kuwa mkikhitalifiana.
 
93Na Mwenyezi Mungu angeli taka, kwa yakini angeli kufanyeni umma mmoja. Lakini anamwachia kupotea anaye mtaka, na anamwongoa amtakaye. Na hakika mtaulizwa kwa yale mliyo kuwa mkiyafanya.
 
94Wala msifanye viapo vyenu ni njia ya kudanganyana baina yenu. Usije mguu ukateleza badala ya kuthibiti, na mkaonja maovu kwa sababu ya kule kuzuilia Njia ya Mwenyezi Mungu, na mkapata adhabu kubwa.
 
95Wala msinunue ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa thamani ndogo. Hakika kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ndicho bora kwenu, ikiwa mnajua.
 
96Mlivyo navyo vitakwisha na vilivyoko kwa Mwenyezi Mungu ndivyo vitakavyo bakia. Na kwa yakini Sisi tutawapa walio subiri ujira wao kwa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda.
 
97Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni Muumini, tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda.
 
98Na ukisoma Qur'ani mwombe Mwenyezi Mungu akulinde na Shetani maluuni.
 
99Hakika yeye hana madaraka juu ya walio amini na wakamtegemea Mola wao Mlezi.
 
100Hakika madaraka yake ni juu ya wanao mfanya rafiki yao, na wale wanao fanya ushirika naye.
 
101Na tunapo badilisha Ishara pahala pa Ishara nyengine, na Mwenyezi Mungu anajua anayo teremsha, wao husema: Wewe ni mzushi. Bali wengi wao hawajui kitu.
 
102Sema: Ameiteremsha hii Roho takatifu kutokana na Mola wako Mlezi kwa haki, ili awathibitishe wale walio amini, na kuwa ni uwongofu, na ni bishara kwa Waislamu.
 
103Na Sisi hakika tunajua kwamba wanasema: Yuko mtu anaye mfundisha. Lugha ya huyo wanaye muelekezea ni ya kigeni, na hii ni lugha ya Kiarabu mbayana.
 
104Hakika wasio ziamini Ishara za Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu hawaongoi, nao watapata adhabu chungu.
 
105Wanao zua uwongo ni wale tu wasio ziamini Ishara za Mwenyezi Mungu. Na hao ndio waongo.
 
106Anaye mkataa Mwenyezi Mungu baada ya kuamini kwake - isipo kuwa aliye lazimishwa na hali ya kuwa moyo wake umetua juu ya Imani, lakini aliye kifungulia kifua chake kukataa - basi hao ghadhabu ya Mwenyezi Mungu ipo juu yao, na wao watapata adhabu kubwa.
 
107Hayo ni kwa sababu wameyapenda zaidi maisha ya duniani kuliko ya Akhera, na kwa sababu Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.
 
108Hao ndio Mwenyezi Mungu ameziziba nyoyo zao na masikio yao na macho yao. Na hao ndio walio ghafilika.
 
109Hapana shaka ya kwamba hao ndio wenye kukhasiri Akhera.
 
110Kisha hakika Mola wako Mlezi, kwa wale walio hama makwao baada ya kuteswa, kisha wakapigania Dini na wakasubiri, bila ya shaka Mola wako Mlezi baada ya hayo ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
 
111Siku ambayo kila nafsi itakuja jitetea, na kila nafsi italipwa sawa sawa na a'mali ilizo zifanya, nao hawatadhulumiwa.
 
112Na Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mji ulio kuwa na amani na utulivu, riziki yake ikiufikia kwa nafasi kutoka kila mahali. Lakini ukazikufuru neema za Mwenyezi Mungu; kwa hivyo Mwenyezi Mungu akauvika vazi la njaa na khofu kwa sababu ya yale waliyo kuwa wakiyafanya.
 
113Na alikwisha wajia Mjumbe wa miongoni mwao wenyewe. Lakini wakamkanusha; basi iliwafika adhabu hali ya kuwa wamedhulumu.
 
114Basi kuleni katika vile alivyo kupeni Mwenyezi Mungu, vilivyo halali na vizuri. Na shukuruni neema za Mwenyezi Mungu, ikiwa kweli mnamuabudu Yeye.
 
115Amekuharimishieni nyamafu tu, na damu, na nyama ya nguruwe, na mnyama aliye chinjwa kwa ajili isiyo kuwa ya Mwenyezi Mungu. Lakini anaye lazimishwa bila ya kuasi, wala kuruka mipaka, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.
 
116Wala msiseme uwongo, kwa kuropokwa na ndimi zenu: Hichi halali, na hichi haramu - mkimzulia uwongo Mwenyezi Mungu. Hakika wanao mzulia uwongo Mwenyezi Mungu hawatafanikiwa.
 
117Ni starehe ndogo, nao watapata adhabu chungu.
 
118Na Mayahudi tuliwaharimishia yale tuliyo kuhadithia zamani. Na Sisi hatukuwadhulumu, bali walikuwa wakijudhulumu wenyewe.
 
119Kisha hakika Mola wako Mlezi kwa walio tenda uovu kwa ujinga, kisha wakatubia baada ya hayo na wakatenda mema; bila ya shaka Mola wako Mlezi baada ya hayo ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.
 
120Hakika Ibrahim alikuwa mfano mwema, mnyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu, mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.
 
121Mwenye kuzishukuru neema zake, Mwenyezi Mungu. Yeye kamteuwa, na akamwongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka.
 
122Na tukampa wema duniani, na hakika Akhera atakuwa miongoni mwa watu wema.
 
123Kisha tukakufunulia ya kwamba ufuate mila ya Ibrahim, mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.
 
124Hakika siku ya Sabato (Jumaamosi) waliwekewa wale walio khitalifiana kwa ajili yake. Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika yale waliyo kuwa wakikhitalifiana.
 
125Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako Mlezi ndiye anaye mjua zaidi aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongoka.
 
126Na mkilipiza basi lipizeni sawa na vile mlivyo adhibiwa. Na ikiwa mtasubiri, basi hakika hivyo ni bora zaidi kwa wanao subiri.
 
127Na subiri. Na kusubiri kwako kusiwe ila kwa sababu ya Mwenyezi Mungu tu. Wala usiwahuzunikie; wala usiwe katika dhiki kwa hila wanazo zifanya.
 
128Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kumcha, na watendao mema.
 
 
ReadTheQuran.org